- Mkuu wa mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo ,amesisitiza kwamba, Tanzania hususan mkoani Pwani ni salama kwa uwekezaji na amekemea propaganda na uvumi unaoenezwa na baadhi ya watu wasiolitakia mema Taifa kuwa hakuna uwekezaji unaoendelezwa.
- Aidha amewaasa ,wawekezaji na wenye viwanda kuhakikisha wanasajili namba za utambulisho ya mlipa kodi (TIN no) kwa meneja wa mamlaka ya mapato (TRA) mkoani hapo ili hali kuongeza pato la mkoa.
- Ndikilo alitoa rai hiyo, wakati alipokwenda kuweka mawe ya msingi katika viwanda vitano vilivyopo wilayani Mkuranga.
- “Rais Dkt.John Magufuli amekuwa akisisitiza uwekezaji na ujenzi wa viwanda kuelekea uchumi wa kati, sasa akitokea mtu kukwamisha jitihada hizo anakuwa halitakii mema Taifa, :”‘Pia mkoa wetu kupitia halmashauri umetenga maeneo hekta 22,937 kwa ajili ya uwekezaji ,nawaomba wawekezaji waje kuwekeza .”alifafanua Ndikilo.
- Hata hivyo, mkuu huyo wa mkoa aliwataka wenye viwanda kujali mikataba,haki,maslahi ya wafanyakazi kwa kuzingatia sheria pamoja na kuwapa likizo na kuwawekea vitendea kazi .
- Awali mkurugenzi wa kiwanda kinachozalisha matofali yenye ubora (Shaffa Ltd) kitongoji cha Kiguza, Suleiman Amour alibainisha ,ujenzi wa kiwanda umeanza 2018 kinatarajia kitakamilika mwaka 2019.
- Amour alisema, lengo la mradi huo ni kuongeza wigo katika sekta ya ujenzi ,na ujenzi utagharimu sh.bilioni 15.3 hadi kukamilika ambapo itatoa ajira 200 mradi ukikamilika.
- Kwa upande wake, msimamizi usafirishaji wa kiwanda cha super meals (Cool Blue) kilichopo Vianzi, Charles Malini alisema, ujenzi wa kiwanda umegharimu bilioni 2.7, kuna ajira 50 ,kinalisha maji ya kunywa ya chupa kwa matumizi ya majumbani na ofisini ambapo wanazalisha ujazo mbalimbali kuanzia nusu lita hadi lita 18.
- Alitaja changamoto zinazowakabili ni kukosa umeme wa uhakika na miundombinu ya barabara isiyo rafiki
- Ndikilo alizungumzia tatizo la barabara na kuwaeleza ,ataangalia namna ya kuingiza hoja hiyo katika kikao cha barabara kijacho ili kiweze kutetea ipandishwe hadhi ihudumiwe na Tanroads.
- Meneja wa shirika la umeme-TANESCO wilayani Mkuranga, Octavian Mmuni alisema tatizo la kukosekana umeme wa uhakika hutokana na maboresho yanayofanyika mara kwa mara.Mmuni alieleza, kwa sasa shirika hilo limetenga sh.milioni 261 ili kusaidia kubadili nguzo na nyaya chakavu.
- Viwanda vingine vilivyowekwa mawe ya msingi katika wilaya hiyo ,ni kiwanda kinachozalisha zana za uvuvi Taxtrade T2 Ltd ,cha nyaya za umeme -Plug Ltd na kiwanda cha kutengeneza masufulia cha Maxima.NA MWAMVUA MWINYI,MKURANGA
Ad