WAZIRI MKUU ASHIRIKI TICAD7- YOKOHOMA, JAPAN IKITOA DOLA BILIONI 20 KUSAIDIA MAENDELEO KWA NCHI ZA AFRIKA

  • Japan imetangaza kutenga kiasi cha dola za kimarekani bilioni 20 kwa kipindi cha miaka mitatu kwa Nchi za Bara la Afrika ili kuziwezesha Nchi hizo kutekeleza miradi ya kimkakati ya maendeleo itakayoleta mageuzi ya kiuchumi katika Bara la Afrika huku Tanzania ikikazia mkakati wake wa uchumi wa viwanda.
  • Waziri Mkuu wa Japan, Mhe. Shinzo Abe ameyasema hayo wakati wa ufunguzi rasmi wa Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (Tokyo Internatinaol Conference on African Development TICAD7) uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Pacifico jijini Yokohama na kuongeza kuwa Serikali ya Japan itaendelea kuchangia maendeleo ya Bara la Afrika kupitia program mbalimbali za ushirikiano kwa kuimarisha rasilimali watu, elimu ya awali kwa watoto na kuboresha huduma ya afya kwa wote.
  • Mhe. Abe amesema kuwa, kupitia Mpango wa TICAD, ushirikiano kati ya Japan na Afrika umeimarika na kwamba nchi hiyo itaendelea kuhakikisha inahamasisha Kampuni za Japan kuwekeza Afrika ambapo hadi sasa sekta binafsi ya Japan imewekeza dola za marekani bilioni 20 katika nchi mbalimbali za Afrika.
PMO 2-01
Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) akisikiliza jambo kutoka kwa Waziri Mkuu wa Mauritius Mhe Pravind Jugnauth. Viongozi wote wawili walikutana na kufanya mazungumzo ya namna ya kuimarisha uhusiano wa kibiashara na kidiplomasia baina ya Nchi hizo. wote wapo katika Mji wa Yokohoma,Japan kushiriki mkutano wa TICAD7.
  • Akizungumzia program mbalimbali zinazotekelezwa na Japan katika kuchangia maendeleo ya Afrika ikiwemo ile ya ABE-African Businness Education Initiative, Waziri Mkuu huyo amesema kuwa tayari vijana zaidi ya 350 kutoka nchi mbalimbali za Afrika wanafanya mafunzo kwa vitendo kwenye Kampuni mbalimbali kupitia mpango huo na wengine 3000 ambao walishapitia mpango huo kama wawezeshaji.
  • Mhe. Abe amesema kuwa, Japan itaendelea kuchangia kwenye sekta ya afya hususan kwenye masuala ya dawa, lishe na kutoa mafunzo ya ujuzi kuhusu masuala hayo kwa nchi mbalimbali za Afrika. Pia Waziri Mkuu huyo amesisitiza kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Afrika kwenye ujenzi wa miundombinu kama barabara na bandari pamoja kutoa wataalam kwani nchi yake haijawahi kupungukiwa wataalam.
  • Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ambaye anahudhuria mkutano huo akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema Tanzania ni miongoni mwa Nchi za Afrika zinazozalisha malighafi zinazosafirishwa nje kwa ajili ya kuongezewa thamani jambo linalofanya Bara la Afrika Tanzania ikiwemo kujikuta ikisafirisha ajira na kutengeneza soko la bidhaa kutoka katika mataifa mengine na kwamba sasa Tanzania imedhamiria kupitia viwanda kutumia malighafi zake kuzalisha bidhaa mbalimbali na hivyo kutengeneza ajira kwa watu wake lakini pia kuuza nje ya nchi na kuzalisha fedha za kigeni.
PMO 3-01
Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) akiwa na Waziri Mkuu wa Mauritius Mhe Pravind Jugnauth walipokutana na kufanya mazungumzo katika mji wa Yokohoma Japan. Kushoto kwa Mhe. Majaliwa ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof Palamagamba John Kabudi (Mb)
  • Ameongeza kuwa kupitia mkakati wa Japan kwa nchi za Afrika Tanzania ni mojawapo ya nchi zitakazonufaika na mkakati huo na kuongeza kuwa mojawapo ya maeneo ya kuboresha ili kufikia azma ya Tanzania ya viwanda ni kujenga miundo mbinu imara itakayoweka msingi wa kufikia malengo hayo kwa kuwezesha usafirishaji wa bidhaa pamoja na malighafi zitakazotumika katika viwanda.
  • Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi amesema tofauti na mikutano iliyotangulia Mkutano huu wa TICAD saba kwa mara ya kwanza umeweka fursa ya kuwa na mpango kazi wa Yokohama ambapo badala ya kuwa na maazimio pekee sasa kutakuwa na fursa ya kuweka malengo vilevile kupima utekelezaji wake na upatikanaji wa fedha.
  • Rais wa Misri, Mhe. Abdel Fattah el-Sisi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika na Mwenyekiti mwenza wa Mkutano wa TICAD 7, Mhe. El-Sisi amesema kuwa Afrika kwa sasa inahitaji mapinduzi katika teknolojia na uvumbuzi ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinalolikabili Bara hilo ikiwemo ukosefu wa ajira kwa vijana na mabadiliko ya tabia. Aidha, ametoa rai kwa nchi zinalizoendelea kutekeleza ahadi zao pamoja na Mkataba wa Paris kuhusu kuzisaidia nchi za Afrika kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi.
PMO 4-01
Waziri Mkuu wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim M. Majaliwa (Mb) akiwa kaaika Mkutano wa Kimataifa Tokyo kuhusu Maendeleo kwa Bara la Afrika. Nyuma yake ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb). Mkutano huo unafanyika Yokohama,Japan.
  • Aidha, Mhe. Rais El-Sisi alitumia fursa hiyo pia kuwakaribisha wawekezaji kutoka Japan kuwekeza Afrika pamoja na kuzitaka taasisi za kifedha za kimataifa kutoa masharti nafuu ya mikopo ili kukuza na kuimarisha uwekezaji na biashara barani Afrika.
  • Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe. Antonio Guteres ameipongeza Japan kwa ushirikiano wake na nchi za Afrika hususan katika kuunga mkono jitihada mbalimbali za kudumisha amani na usalama baranii humo. Pia amezipongeza nchi za Afrika kwa kuanzisha Mpango wa Eneo Huru la Biashara barani humo ambao kwa kiasi kikubwa utaimarisha sekta ya biashara na uwekezaji na kuchangia maendeleo ya nchi hizo. Mhe. Guteres amesisistiza kuwa nchi za Afrika kwa kushirikiana na Japan ziwekeze kwenye elimu bora kwa vijana hususan kwenye maeneo ya sayansi, hesabu na teknolojia kwani yana mchango mkubwa katika maendeleo.
  • Akizungumzia mabadiliko ya tabianchi, Mhe. Guteres amesema kuwa jitihada za pamoja zinahitajika ili kukabiliana na changamoto zitokanazo na mabadiliko hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yanaziathiri nchi za Afrika. Katibu Mkuu huyo aliongeza kuwa ameitisha Mkutano kuhusu mabadiliko ya tabianchi utakaofanyika jijini New York, Marekani mwezi Septemba 2019 ili kwa pamoja nchi zijadili namna ya kuendelea kutatua changamoto hizo.
  • Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Mhe. Moussa Faki Mahamat ambao hushirikiana na Japan kuandaa mikutano ya TICAD, amesema kuwa, Mkutano wa Saba umekuja na suluhisho kwa vijana kuhusu masuala ya teknolojia na uvumbuzi na kusisistiza kwamba suala hilo ni la kipaumbele kwa nchi za Afrika.
  • Mkutano wa Saba wa TICAD ambao umebeba kaulimbiu ya Kuiendeleza Afrika kupitia Watu, Teknolojia na Uvumbuzi, umehudhuriwa na zaidi ya washiriki 4,000 pamoja na Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka nchi 44 za Afrika.

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,

Ad

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Yokohama, Japan.

28 Agosti 2019

Ad

Unaweza kuangalia pia

WAZIRI ZUNGU AHUDHURIA MKUTANO WA 7 WA BARAZA LA KISEKTA LA MAWAZIRI WA MAZINGIRA NA MALIASILI WA JUMUIA YA AFRIKA MASHARIKI

             

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *