- Serikali imefanya ukaguzi wa upatikanaji wa huduma za mawasiliano mkoani Kigoma na kuridhishwa na hali ya mawasiliano mkoani humo kwa kubaini kuwa wananchi wanapata huduma za mawasiliano na wanawasiliana kwa kutumia mitandao ya kampuni za simu iliyopo
- Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye amesema kuwa ameridhishwa na huduma ya mawasiliano iliyopo mkoani Kigoma wakati wa ziara yake mkoani humo ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwenye maeneo ya Kigoma mjini, Chankere, Mwamgongo, Kagunga, Ruhita, Mrufiti na Kasulu
- Nditiye amebaini kuwa mawasiliano ya simu za mkononi yanapatikana na wananchi wanawasiiana wakati alipokuwa anakagua upatikanaji wa mawasiliano kwenye eneo la Kagunga ambalo liko kwenye mwiniko na mlima mkali ambapo inafanya eneo hilo kuwa na umbali wa futi 1,700 kutoka usawa wa bahari ambazo ni zaidi ya futi 1,000 kutoka Kigoma mjini ambapo kuna futi 700 tu kutoka usawa wa bahari
- “Pamoja na kuwa na umbali wa kiasi na uwepo wa changamoto ya barabara ya kutoka Kanchere hadi Kagunga ila bado mawasilino yanapatikana ya zaidi ya kampuni moja ya simu za mkononi, niwapongeze Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote,” amesema Nditiye wakati akiwa eneo hilo la Kagunga.
- “Nimekuja makusudi kushuhudia wananchi wanatumia huduma hii,” amesisitiza Nditiye. Akiwa Kagunga, Nditiye amefafanua kuwa eneo hilo lina mtandao zaidi ya miwili na mawasiliano yanapatikana. Ameongeza kuwa lengo ni kuhakikisha kuwa wanamsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanznia, Dkt. John Pombe Magufuli kuhakikisha kuwa wananchi wanatumia huduma za mawasiliano. Nuhu Nuru Suedi, mmoja wa wananchi waishio eneo hilo, akizungumza kwa niaba ya wenzake, amesema kuwa mawasiliano yanapatikana vizuri na yanawawezesha kupeana taarifa kwa wakati na kwa urahisi inapotokea dharura ya mgonjwa
- Naye Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Bi. Justina Mashiba wakati akizungumza na wanachi amesema kuwa UCSAF ina minara 29 mkoani Kigoma na tayari minara 27 imewashwa na inafanya kazi ya kutoa huduma za mawasiliano kwa wananchi. Mashiba amesema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa wananchi wake waishio vijijini wanapata huduma za mawasiliano kwa kuwa ni watanzania wenzetu
- Mashiba amesema kuwa Ruhita ni moja ya Kata iliyonufaika na ujenzi wa mnara wa mawasiliano kupitia UCSAF kwa kujengewa mnara kupitia ruzuku inayotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia, amewataka wananchi kuilinda na kuitunza miundombinu ya mawasiliano kwa kuwa ujenzi wa miundombinu hiyo inatokana na kodi za wananchi ambazo Serikali imezikusanya.
- Akiwa ofisini kwake, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga amemuomba Nditiye kuhakikisha kuwa wananchi waishio Kigoma wanapata mawasiliano ya uhakika kwa kuwa baadhi ya maeneo ya Kigoma yanapakana na nchi jirani za DRC Congo na Burundi hivyo haitakuwa vizuri watanzania waishio maeneo ya mipakani wapate mawasiliano ya simu na redio ya kutoka nchi jirani
- Katika ziara hiyo, Nditiye amehamasisha wananchi wasajili laini zao za simu za mkononi kwa kutumia alama ya vidole ili waweze kutambulika. Nditiye ameambatana na Mkuu wa Kanda ya Kati ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Antonio Manyanda na wataalamu wengine ili kuelimisha umma kuhusu usajili wa laini za simu za mkononi, manufaa ya anwani za makazi na postikodi na kukagua miundombinu na upatikanaji wa huduma za mawasiliano mkoani humo
Ad