RAIS DKT. MAGUFULI APOKEA HATI ZA UTAMBULISHO TOKA KWA MABALOZI WAPYA WA FINLAND, UMOJA WA ULAYA NA RWANDA

  • Rais Dkt. John  Magufuli amepokea hati za utambulisho za Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) hapa nchini Mhe. Manfred Fanti, Balozi wa Finland hapa nchini Mhe. Riitta Swan na Balozi wa Rwanda hapa nchini Mhe. Mej. Jen. Charles Karamba, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
  • Akizungumza na Mhe. Rais Magufuli baada ya kuwasilisha hati zake za utambulisho Mhe. Balozi Manfred Fanti ameishukuru Tanzania kwa kumpokea kuja kuiwakilisha EU hapa nchini na amesema katika kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano na EU na Tanzania atajielekeza zaidi katika masuala ya maendeleo kwa kuwa anaamini kuna mambo mengi na mazuri ya kufanya yatakayoiwezesha Tanzania kuingia katika uchumi wa kati kama ilivyopanga.
6-01
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akifanya mazungumzo na Balozi mteule wa Umoja wa Ulaya (EU) Mhe. Manfredo Fanti baada ya kupokea hati yake ya utambulisho kwenye hafla fupi iliyofanyika Ikulu jijini Dar es salaa leo Jumatatu Oktoba 28, 2019
  • Mhe. Balozi Fanti ameongeza kuwa anaamini katika mazungumzo ya pamoja kati ya Tanzania na EU katika masuala mbalimbali na kwamba katika kipindi chake anatarajia kutilia mkazo miradi ya kuzalisha nishati ya umeme kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na utekelezaji wa miradi mingine iliyopo katika makubaliano ya 11 ya mkataba wa mfuko wa maendeleo ya EU uliotengewa shilingi Trilioni 1.583 yanatekelezwa.
  • Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mhe. Balozi Fanti kwa msimamo wake wa kuimarisha na kukuza zaidi uhusiano wa Tanzania na EU na amesema Tanzania inatambua uhusiano mzuri na wa kihistoria uliopo kati yake na EU na kwamba ipo tayari kushirikiana na Balozi huyo katika utekelezaji wa masuala yenye maslahi kwa pande zote mbili.
5-01
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipokea hati ya utambulisho toka kwa Balozi mteule wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Mhe. Manfredo Fanti kwenye hafla fupi iliyofanyika Ikulu jijini Dar es salaa leo Jumatatu Oktoba 28, 2019
  • Kwa upande wake Balozi wa Finland hapa nchini Mhe. Riitta Swan pamoja na kushukuru kwa kupokelewa amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa mafanikio makubwa katika kupambana na rushwa na amesema katika kipindi chake hapa nchini atahakikisha maeneo ya uhusiano kati ya Tanzania na Finland yanaimarishwa ikiwemo mradi wa utunzaji wa mazingira, kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa kodi kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na utawala bora.
  • Mhe. Rais Magufuli amemshukuru kwa dhamira yake ya kukuza zaidi ushirikiano na uhusiano na Tanzania na amesema Tanzania itakuwa tayari kutoa ushirikiano wowote atakaouhitaji.
4-01
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Balozi wa Jamhuri ya Finland nchini Mhe. Riita Swan baada ya kupokea hati yake ya utambulisho kwenye hafla fupi iliyofanyika Ikulu jijini Dar es salaa leo Jumatatu Oktoba 28, 2019
  • Nae Balozi wa Rwanda hapa nchini Mhe. Mej. Jen. Charles Karamba ameishukuru Tanzania kwa kumkaribisha na amemhakikishia Mhe. Rais Magufuli kuwa katika kipindi chake cha Ubalozi atahakikisha matarajio ya Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame kukuza zaidi uhusiano wa Tanzania na Rwanda yanafanikiwa.
  • Mhe. Rais Magufuli amemkaribisha Mhe. Balozi Karamba na kumtaka ahakikishe biashara kati ya Tanzania na Rwanda inakuwa zaidi ikiwemo kutekelezwa kwa makubaliano yake na Mhe. Rais Kagame ya Rwanda kutumia bandari ya Tanga katika upokeaji na usafirishaji wa mizigo ya kwenda na kutoka Rwanda.
3-01
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipokea hati ya utambulisho toka kwa Balozi mteule wa Jamhuri ya Finland nchini Mhe. Riita Swan kwenye hafla fupi iliyofanyika Ikulu jijini Dar es salaa leo Jumatatu Oktoba 28, 2019
  • “Sisi ni ndugu na ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mwenyekiti wetu ni Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame, hatuna sababu ya kupoteza muda, nataka usukume sana suala la kuongeza biashara kati ya Tanzania na Rwanda ili nchi zetu zinufaike zaidi” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
1-01
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipokea hati ya utambulisho toka kwa Balozi mteule wa Jamhuri ya Rwanda nchini Meja Jenerali Charles Karamba kwenye hafla fupi iliyofanyika Ikulu jijini Dar es salaa leo Jumatatu Oktoba 28, 2019
Ad

Unaweza kuangalia pia

LIVE: UZINDUZI WA MAJENGO YA OFISI YA MANISPAA NA MKUU WA WILAYA KIGAMBONI JIJINI DSM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 11, Febuari, …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *