BODI YATOA TATHMINI KUHUSU UTEKELEZWAJI MIRADI YA UMEME VIJIJINI MOROGORO

  • Kamati ya Ufundi ya Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Oktoba 25, mwaka huu ilikabidhi kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Olesanare, taarifa ya tathmini kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini mkoani humo, baada ya ziara yao ya siku mbili.
  • Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhandisi Styden Rwebangila, alisema, ripoti waliyoikabidhi kwa Mkuu wa Mkoa inalenga kumpatia uelewa wa miradi ya umeme vijijini inayotekelezwa katika mkoa wake ili aweze kujua kinachoendelea akiwa ndiye msimamizi mkuu wa utekelezaji wa shughuli za serikali mkoani humo.
33-01
Matukio mbalimbali wakati Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Olesanare, alipokuwa akizungumza na Ujumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), ofisini kwake
  • “Unajua Mkuu huyu wa Mkoa hana muda mrefu tangu alipoteuliwa na Mheshimiwa Rais John Magufuli kushika wadhifa huo, hivyo anapaswa kujengewa uelewa wa kila kinachoendelea mkoani kwake,”amefafanua Rwebangila.
  • Akieleza kuhusu tathmini hiyo, Rwebangila alisema kuwa kwa ujumla, Kamati yake imebaini hali ya utekelezaji wa mradi husika mkoani humo hairidhishi.
  • “Hii ni kwa sababu, mpaka sasa, mkandarasi M/s State Grid Electrical Works, amewasha umeme katika vijiji 38 tu kati ya 165 vya kimkataba sawa na asilimia 23 ya utekelezaji. Aidha, ameunganisha wateja 841 kati ya 10,457 wa kimkataba, sawa na asilimia nane pekee.”
44-01
Matukio mbalimbali wakati Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Olesanare, alipokuwa akizungumza na Ujumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), ofisini kwake
  • Alisema Ujumbe wa Bodi umegundua mapungufu mbalimbali ambayo ni pamoja na mkandarasi kutokuwa na magenge ya kutosha pamoja na kuwa na upungufu wa nguzo takribani 5,704 hivyo kuzorotesha kazi za usimikaji wake.
  • Mengine ni kuwa na upungufu wa nyaya za umeme wa msongo wa kati na mdogo wa jumla ya kilomita 760, kufikisha eneo la kazi transfoma 87 tu kati ya 288 zilizopo kwenye mkataba hivyo kusababisha upungufu wa transfoma 201  na kuzorotesha kazi ya kuunganisha wateja.
55-01
Ujumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), ukiwa katika kikao cha ndani na Mameneja wa TANESCO wa Mkoa wa Morogoro na wa Wilaya zake zote, pamoja na Mkandarasi anayetekeleza mradi wa umeme vijijini mkoani humo
  • Vilevile, mkandarasi ametelekeza baadhi ya nguzo chini pasipo kuzichimbia pamoja na uwepo wa wateja waliolipia huduma lakini hawajaunganishiwa umeme.
  • Kutokana na mapungufu hayo, Bodi imemwagiza mkandarasi kuhakikisha nguzo zote ambazo ziko chini zinajengwa ndani ya siku 14 kuanzia Oktoba 24, 2019. Aidha, wateja wote waliolipia wawe wameunganishiwa umeme na kuvuta nyaya zote zilizopo eneo la mradi ndani ya muda huo.
11-01
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Olesanare akizungumza na Ujumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (hawapo pichani), ofisini kwake
  • Maagizo mengine yaliyotolewa na Bodi ni mkandarasi kuhakikisha kabla ya Novemba 30 mwaka huu, awe amepeleka nyaya zote zenye jumla ya urefu wa kilomita 760 na kujenga, apeleke transfoma zote 201 zilizosalia katika maeneo ya mradi na kuzifunga na apeleke nguzo zote 5,704 zilizobaki katika maeneo ya mradi na kuzijengea.
  • Aidha, mkandarasi ametakiwa kuhakikisha magenge yanaongezwa na kufikia matano kwa kila wilaya ndani ya siku saba pamoja na kuhakikisha kuwa wateja wote ambao hawana uwezo wa kumudu gharama za kutandaza mfumo wa nyaya (wiring), wanaunganishiwa umeme kwa kutumia kifaa cha Umeme Tayari (UMETA).
  • Mradi huo unatekelezwa katika wilaya sita za mkoa wa Morogoro ambazo ni Kilombero, Mvomero, Ulanga, Gairo, Kilosa na Morogoro Vijijini.Na Veronica Simba – Morogoro
Ad

Unaweza kuangalia pia

TPDC YAOKOA TRILIONI 12.7 KUAGIZA MAFUTA NJE YA NCHI

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *