- Mke wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa ametoa wito kwa wazazi na walezi watoto wenye mahitaji maalumu kutowaficha na kuwatelekeza na badala yake wawape nafasi ya kupata elimu kwa sababu ni haki yao ya msingi.
- Mama Majaliwa ambaye pia ni Mlezi wa Umoja wa Wake wa Viongozi (New Mellenium Women Group), ametoa wito huo (Jumapili, Novemba 10, 2019), wakati alipokabidhi majengo ya madarasa manne na matundu ya vyoo kumi kwa Kituo cha Watoto Wenye Ulemavu cha Buhangija mkoani Shinyanga yaliyojengwa na umoja huo.
- Mama Majaliwa amesema si vyema kuwatenga au kuwakatia tamaa watoto wenye ulemavu kwani wao pia ni watoto sawa na watoto wengine, hivyo wanastahili kupewa haki zote bila kubaguliwa.
- Amesema hatua waliyochukuwa akinamama wa umoja huo inaunga mkono jitihada za serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli za kuwapatia watoto wa kitanzanai elimu bure na katika mzingira mazuri.
- Mgeni rasmi katika makabidhiano hayo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Profesa, Joyce Ndalichako ameupongeza umoja huo kwa shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kuwajali watoto wenye mahitaji maalumu.
- Profesa Ndalichako amesema katika kipindi cha mwaka 2019/2020 Serikali imetenga jumla ya sh 3,809,758,460.00 kwa ajili ya kununua na kusambaza vifaa vya kufundishia na kujifunzia pamoja na vifaa visaidizi kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum (wakiwemo Albino), katika shule na vitengo vya elimu maalum.
- Waziri huyo ameongeza kuwa pamoja na juhudi hizo za Serikali, bado wanafurahi wanapopata michango kama huo uliotolewa leo. “Wito wangu kwenu tusichoke kuwasaidia hawa watoto wetu. Napenda kuwakumbusha na kusisitiza kwamba Watu wenye Ulemavu wanahitaji msaada mkubwa kutoka kwenu.”
- “Tuwasaidie na tushirikiane kuwapatia mahitaji yao muhimu ikiwa ni pamoja na elimu, huduma za afya na mazingira mazuri ya kuwawezesha kuishi bila ya matatizo. Serikali kwa upande wake itaendelea kujitahidi kwa uwezo kutoa fursa zinazojali mahitaji yao.”
- Amesema madarasa pamoja na vyoo alivyokabidhiwa leo kwa niaba ya uongozi wa kituo cha Buhangija na Kikundi cha New Millenium ni tunu kwao na wananchi wa Shinyanga na ni sadaka kwa watoto wa Buhangija, hivyo, ameutaka uongozi wa Mkoa na Uongozi wa Kituo kwa pamoja washirikiane kuyatunza vizuri ili yaweze kutumika kwa muda mrefu.
- Akitoa taarifa ya ujenzi huo kwa mgeni rasmi, Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela amesema fedha zilizotumika kwa ajili ya ujenzi wa madarasa manne ni sh. 65m,884,523/= ambapo kila chumba cha darasa kimejengwa kwa wastani wa sh. 16,471,130.
- Amesema ujenzi wa vyumba kumi vya vyoo unaendelea na ukikamilika utagharimu sh.26, 271,922.44 na kwamba vyoo hivyo vitakuwa vya kisasa vikiwa na maji ndani pamoja na masinki ya kunawia ili kukidhi mahitaji ya watoto wenye ulemavu.
Ad