- Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Biashara Mashariki na Kusini wa Afrika (TDB) Bw. Admassu Tadesse, ambapo Benki hiyo imeahidi kuipatia Tanzania mkopo wenye masharti nafuu wa dola milioni 200 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
- Mazungumzo ya viongozi hao yamefanyika katika Mji wa Sandton, Johannesburg nchini Afrika Kusini, kando ya Kongamano la Pili la Jukwaa la Uwekezaji Afrika lililoandaliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB.
- Dkt Mpango amesema kuwa Benki hiyo imekuwa mbia mzuri wa Tanzania ambapo mwaka huu pekee imetoa mkopo wa dola bilioni 1 kwa ajili ya miradi ya maendeleo na imeahidi kutoa kiasi kingine cha dola milioni 200 baada ya Bodi ya Benki hiyo kukutana mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka huu kwa ajili kuidhinisha mkopo huo
- Alisema kuwa amemwalika Rais huyo wa Benki ya Maendeleo ya Biashara Bw. Tadesse, kufanya ziara ya kikazi nchini Tanzania hivi karibuni ili kujionea miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ukiwemo mradi wa kuzalisha umeme wa Kilwa pamoja na miradi mingine ambayo Benki hiyo inaweza kutoa mkopo
- Kwa upande wake, Rais wa TDB Bw. Admassu Tadesse amesifu uhusiano imara uliopo kati ya Benki yake na Serikali ya Tanzania na kuahidi kuwa Benki hiyo itahakikisha inashirikiana nayo kwa ajili ya kuharakisha maendeleo ya wananchi wake.
- “Tumekuwa na mjadala mzuri na Mhesimiwa Dkt. Mpango na Benki yetu imekuwa mshirika mzuri wa maendeleo ya Tanzania katika kipindi cha miaka michache iliyopita kwenye yyanja za nishati ya umeme na miundombinu ya usafirishaji” alisema Bw. Tadesse
- Alisema kuwa mwaka huu Benki yake kwa kushirikiana na washirika wake wengine ambao ni taasisi za kibenki imeongeza mtaji wa dola milioni 500 hatua iliyoijengea Benki yake uwezo wa kutoa mikopo zaidi ambapo mwakani itaipatia mikopo kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya kimkakati ya miundombinu itakayokuwa na umuhimu mkubwa si tu kwa Tanzania, bali pia kikanda.
- Benki ya Biashara na Maendeleo ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (TDB) ilianzishwa mwaka 1985 ikiwa na mali zenye thamani ya dola za Marekani bilioni 5.6 ambapo lengo lake kubwa ni kutoa mikopo inayochochea miradi inayochochea ukuaji wa biashara, ikiwemo miundombinu, utangamano wa kiuchumi na ushauri wa kibiashara kwa nchi wanachama. Na Benny Mwaipaja, Johannesburg
Ad