- Kwa kipindi cha miaka minne Serikali imeweza kuokoa zaidi ya shilingi bilioni 89 kwa wagonjwa 5954 wenye matatizo makubwa ya moyo ambao walifanyiwa upasuaji wa kufungua na bila kufungua kifua katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
- Kama wagonjwa hawa 5954 waliofanyiwa upasuaji hapa nchini wangetibiwa nje ya nchi Serikali ingetumia zaidi ya shilingi bilioni 178 kulipia gharama za matibabu hayo.
- Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi wakati akielezea mafanikio ya miaka minne ya Serikali ya awamu ya tano kwa upande wa matibabu ya moyo katika kikao cha bodi ya wadhamani ya Taasisi hiyo.
- Prof. Janabi alisema kwa wagonjwa hao kutibiwa hapa nchini matibabu yao yamegharimu kiasi cha shilingi bilioni 89 fedha ambazo zimelipwa kupitia bima zao za matibu, misaada ya wafadhili mbalimbali wa nje, wagonjwa wenyewe kujilipia na Serikali kugharamia matibabu ya wagonjwa wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za matibabu.
- “Gharama ya mgonjwa mmoja aliyefanyiwa upasuaji nje ya nchi ni zaidi ya shilingi milioni 30, lakini kwa mgonjwa mmoja kutibiwa hapa nchini gharama zake hazizidi shilingi milioni 15. Kwa kutibiwa hapa nchini fedha anazolipa mgonjwa zinatumika kununua vifaa tunavyomuwekea katika moyo wake kama vile pacemaker, high power device, stent, device closure na valvu vifaa hivi tunaviagiza nje ya nchi kwani hazipatikani hapa nchini”, alisema Prof. Janabi.
- Mkurugenzi huyo Mtendaji aliendelea kusema kwa kipindi cha miaka minne wameweza kuona wagonjwa 300,836 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani pamoja na nchi jirani kama vile Demokrasia ya Congo, Malawi, Ethiopia, Zambia, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Visiwa vya Comoro.
- “Jambo la kufurahia ni kuwa tumeweza kuokoa maisha ya watu ambao tumewatibu na hivi sasa wanaendelea na majukumu yao ya kazi za kila siku. Kwa kipindi cha miaka minne tulilaza wagonjwa 14,960 tumefanya upasuaji wa bila kufungua kifua kwa kutumia mtambo wa Cathlab kwa wagonjwa 4,207 na upasuaji wa kufungua kifua na kusimamisha moyo kwa wagonjwa 1,747”,alisema Prof. Janabi.
- Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi hiyo ambayo inamaliza muda wake Prof. William Mahalu aliupongeza uongozi wa Taasisi hiyo pamoja na wafanyakazi kutokana na huduma za matibabu ya moyo wanazozitoa kwa wagonjwa wanaowatibu.
- Prof. Mahalu ambaye ni mmoja wa madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa kwanza hapa nchini alisema anamaliza muda wake kama Mwenyekiti wa bodi hiyo huku ndoto yake ya kuona Tanzania inakuwa na Hospitali ya matibabu ya moyo ikiwa imetimia.
- “Ninamshukuru sana Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuniteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini ya Taasisi hii kwa kipindi cha miaka mitatu. Kama mtakumbuka tangu nchi yetu ipate Uhuru mwaka 1961 wananchi wengi wenye matatizo ya moyo yaliyohitaji kufanyiwa matibabu ya kibingwa iliwalazimu kwenda kutibiwa nje ya nchi.
- “Kwa kuwa kutibiwa nje ya nchi ni gharama na pia mlolongo kuwa mrefu baadhi ya wagonjwa walipoteza maisha wakati wakisubiri fedha za kwenda kupata matibabu. Hivi sasa wananchi hawapati tabu tena wanatibiwa hapa nchini kwa wakati. Ukiangalia idadi ya wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi yetu imeongezeka kutoka wagonjwa 150 kwa mwaka 2016 hadi kufikia wagonjwa 300 kwa siku kwa mwaka 2019”, alisema Prof. Mahalu.
- Prof. Mahalu alisema wakati anasomea upasuaji wa moyo nje ya nchi kuna daktari alimkatisha tamaa na kumwambia kuwa hawataweza lakini hakukata tamaa alihakikisha anasoma kwa bidii na baada ya kuhitimu masomo yake aliweza kufanya upasuaji na alimualika yule daktari aliyemkatisha tamaa kwenda kushuhudia jinsi wanavyofanya upasuaji.
- Aidha Prof. Mahali aliwashukuru wajumbe wa Bodi ya wadhamini kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kuhakikisha Taasisi ya Moyo inafanya kazi zake za kutoa huduma kwa wananchi kwa weledi na wakati.
- Bodi ya Wadhamini ya Taasisi hiyo ambayo imemaliza muda wake jana tarehe 13/11/2019 kwa kufanya kazi kwa kipindi cha miaka mitatu ilizinduliwa na Mhe. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu tarehe 21 Machi 2017.
Ad