WATUMISHI FANYENI KAZI KWA UADILIFU, UTIIFU NA WELEDI – SHIGELA

  • Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela amewataka watumishi wa Umma kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya utumishi, Uadilifu, utiifu, weledi, taratibu na sheria za kazi katika kutumiza majukumu yao kila siku.
  • Shigela alisema hayo, Novemba 14, 2019 kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Utumishi, Dkt. Laurian Ndumbaro, wakati akifungua Kikao kazi cha  Wakurugenzi,Mameneja wa Utawala na Usimamizi wa  Rasilimali watu wa Wizara ya Nishati na Taasisi zilizochini yake kilichofanyika mkoani Tanga.
2-01
Mkuregenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO), Dkt.Tito Mwinuka( katikati) akizungumza wakati akifungua Kikao kazi cha Wakurugenzi,Mameneja wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Wizara ya Nishati na Taasisi zilizochini yake kilichofanyika mkoani Tanga.
  • Akizungumza katika kikao hicho, Shigela aliwaeleza washiriki wa mkutano huo kuwa pia wanatakiwa kufanya kazi kwa kutumia Lugha safi na sahihi kulingana na huduma wanayoitoa kwa mtumishi au mteja katika eneo husika.
  • Alisema endapo Wakurugenzi na Mameneja wa Rasilimaliwatu  watafanya kazi zao kwa misingi inayotakiwa, hakika kazi zote na miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali itafanyika kwa umakini mkubwa na kukamilika kwa wakati.
  • Vilevile itasaidia wao pamoja na watumishi na wafanyakazi waliochini yao kujilinda na kuwaepusha na vishawishi dhidi ya rushwa katika sehemu zao za kazi.
3-01
Mkurugenzi Mkuu wa Utawala na Rasilimaliwatu wa Wizara ya Nishati, Raphael Nombo,(kulia) na Katibu wa Sekterarieti ya Ajira Xavier Daudi(kushoto) wakisoma nyaraka wakati wa Kikao kazi cha Wakurugenzi,Mameneja wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Wizara ya Nishati na Taasisi zilizochini yake kilichofanyika mkoani Tanga.
  • Alifafanua kuwa Wakurugenzi na Mameneja ndiyo wenye dhamana kubwa ya kusimamia watendaji na watumishi walio chini yao sehemu za kazi, hivyo wanapaswa kutimiza majukumu kwa weledi ili kuwawezesha watumishi wanaowaongoza kutekeleza majukumu  kwa ufanisi na bila malalamiko.
  • Aidha, Shigela aliipongeza Wizara ya Nishati, kwa kuwa wizara ya kwanza kutekeleza agizo la Katibu Mkuu, ofisi ya Rais, Utumishi lililoelekeza wizara zote nchini kuweka utaratibu wa kufanya vikao kazi na taasisi zilizochini yake ili kubaini changamoto na kuboresha mambo mbalimbali katika Utendaji kazi na usimamizi wa Rasilimaliwatu.
5-01
Meneja Mwandamizi Rasilimaliwatu wa Shirika la Umeme Tanzania( Tanesco), Francis Sangunaa,(katikati) akiwasilisha nyaraka wakati wa kikao kazi cha Wakurugenzi,Mameneja wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Wizara ya Nishati na Taasisi zilizochini yake, mkoani tanga . Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi sehemu ya Utawala wa Wizara ya Nishati , Daniel Machunda na Meneja Mkuu( TANOIL) Kampuni Tanzu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania ( TPDC)inayoshughulikia uwekezaji katika sekta ya mafuta, Mhandisi Kapuulya Musomba(kushoto)
  • “Watumishi wa umma wanahitaji kusikilizwa na kutatuliwa changamoto zao, kwa kuwa wao ni kiungo muhimu cha kufinikisha na kuwafikia wananchi moja kwa moja yale mengi mazuri  yanayotekelezwa na serikali kwa wananchi wake, pia  ni watu wanaotumia muda kazini kuliko katika familia zao, hivyo wasiposimamiwa vizuri na kupata miongozo sahihi , yale mazuri yanayofanywa na serikali hayata wafikia wananchi kama inavyotakiwa”, alisisitiza Shigela.
  • Akizungumzia suala la kuwaongezea uwezo watendaji na watumishi, Shigela alizishauri Wizara na Taasisi mbalimbali kuweka utaratibu wa kuwapatia mafunzo ya mara kwa mara watumishi wao ili kuendana na teknolojia inayokuwa kila siku na kuwapa motisha kazini.
  • Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Dkt.Tito Mwinuka, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt.Khamis Mwinyimvua,  alisema kuwa utaratibu wa kufanya vikao na kuzungumza na Tasisi zilizochini ya Wizara imesaidia sana kuongeza ushirikiano kati ya mtumishi na muajiri.
6-01
Washiriki wa Kikao kazi cha Wakurugenzi, Mameneja wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Wizara ya Nishati na Taasisi zilizochini yake wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Martin shigela( katikati mbele) wakati wa kikao hicho kilichofanyika mkoani humo.
  • Pia vimesaidia kutatua changamoto mbalimbali zilizokuwa  zinawakabili wafanyakazi na watumishi ikiwemo kuondoa ama kupunguza malalamiko kati ya wafanyakazi na waajiri katika maeneo ya kazi.
  • Vilevile, imeboresha na kuinua ari ya utendaji kazi kwa watumishi na wafanyakazi wa maeneo husika kwa kuwa haki zao za msingi zinatatuliwa wakati sahihi.
  • Sambamba na hilo, Dkt.Mwinuka alisema kuwa imesaidia wafanyakazi na watumishi wengi kuzungumza na kuweka wazi changamoto zinazowakabili kwa kuwa zinasikilizwa, na kupatiwa majawabu  pamoja na kuelezwa  hatua zinazochukuliwa dhidi ya changamoto hizo kabla ya kutatuliwa.
7-01
Afisa Utumishi wa Wizara ya Nishati, Mwanaid Ghasia( katikati) akisikiliza mada wakati wa wa Kikao kazi cha wakurugenzi, Mameneja wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Wizara ya Nishati na Taasisi zilizochini yake kilichofanyika mkoani Tanga.
  • “Utaratibu huu ni mzuri sana umeleta matokeo chanya, Taasisi na Wizara tunajua uhitaji na changamoto zinazowakabili wafanyakazi na watumishi wa sekta zetu kila inapotea, na tunafahamu ni namna gani tunazishughulikia kwa pamoja na kwa haraka zaidi tofauti na ilivokuwa huko nyuma, naupongeza sana huu utaratibu” alisema Dkt. Mwinuka.
  • Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Utawala na Usimamizi  wa Rasilimaliwatu wa  Wizara ya Nishati, Raphael Nombo, alimshukuru Mkuu wa Mkoa huyo na kumuhakikishia kuwa wao kama wasimamizi wa watumishi na wafanyakazi katika Wizara, Taasisi na Idara mbalimbali  za Serikali watafanya kazi zao kwa uadilifu, weledi,ubunifu na kujituma kwa kuzingatia misingi na taratibu za kazi.
4-01
Mkurugenzi Mkuu wa Utawala na Rasilimaliwatu wa Wizara ya Nishati, Raphael Nombo,(kulia)akibadilishana jambo na viongozi wengine mara baada ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela(katikati) kufungua kikao kazi cha Wakurugenzi,Mameneja wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Wizara ya Nishati na Taasisi zilizochini yake kilichofanyika mkoani humo.kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka.
  • Alienda mbali zaidi kwa kusema kuwa, Wizara ya Nishati ni moja ya nguzo kubwa na muhimili muhimu Sana katika kuchangia maendeleo ya uchumi kwa kuwezesha kupatikana kwa Nishati ya Umeme nchi nzima, hivyo wanajukumu kubwa la kuwasimamia vyema watendaji, watumishi na wafanyakazi ili na wao wafanye kazi zao kwa weledi ,kujituma, ubunifu kwa maslahi  makubwa ya Taifa.
  • “Azma  ya Serikali ya Awamu ya Tano kujenga uchumi wa viwanda kila kona ya nchi yetu, Wizara ya Nishati,  sisi ndiyo tunadhamana kubwa sababu tunazalisha umeme unaotumika katika viwanda hivyo, tunawahakikishia watanzania kuwa tunatekeleza majukumu yetu usiku na mchana bila kuchoka kuhakikisha umeme mwingi na wakutosha unapatikana  wakati wote katika maeneo ya uzalishaji hasa viwandani kutimiza lengo lililokusudiwa,” alisisitiza Nombo.
  • Nombo alisema kuwa hicho ni kikao cha tatu kufanyika ambapo kikao cha kwanza kilifanyika Mikoani Dar ES salaam, cha pili mkoani Mwanza, ambavyo vinafanyika kila robo mwaka,  ikiwa ni utaratibu waliojiwekea katika wizara hiyo na Tasisi zake ili kuzungumza  na kujadili mambo kadha yanayojikeza kwa lengo la kuboresha utendaji kazi na kutatua changamoto endapo zimejitokeza.
Ad

Unaweza kuangalia pia

TPA YAWEKA MIUNDOMBINU BANDARI YA ZIWA NYASA KUHAKIKISHA WANANCHI WANAPATA HUDUMA YA USAFIRI

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania(TPA) imesema imeshaweka miundombinu katika bandari za Ziwa Nyasa kwa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *