- Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeeleza kuridhishwa kwake na utekelezaji wa maagizo iliyoyatoa kwa Mkandarasi anayefanya kazi ya kusambaza umeme vijijini wilayani Chato kampuni ya Whitecity Guangdong JV ambayo yalilenga kuongeza kasi ya usambazaji umeme vijijini.
- Hayo yalielezwa na Mwenyekiti wa Bodi ya REA, Wakili Julius Kalolo tarehe 17 Novemba, 2019, wilayani Chato, Mkoa wa Geita mara baada ya kukagua kazi za usambazaji umeme zinazoendelea wilayani humo akiwa ameambatana na Mjumbe wa Bodi hiyo, Dkt Andrew Komba na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga.
- Alieleza kuwa, maagizo ya Bodi hiyo yalitolewa Siku 14 zilizopita ambapo Mkandarasi huyo alielekezwa kutekeleza kazi ambazo alikuwa hajafanya kwenye baadhi ya maeneo ikiwemo kuchimba mashimo, kusimika nguzo na kuvuta nyaya ili kuweza kuwasha umeme katika Vijiji alivyopangiwa kupitia mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu Mzunguko wa kwanza (REA III).
- ” Tulitoa maagizo haya Wiki mbili zilizopita baada ya kufanya ziara wilayani hapa na kukuta nguzo zimelala na Mkandarasi alikuwa haonyeshi kama alikuwa na uwezo wa kufanya kazi kwa kasi tunayotaka lakini baada ya kukagua leo tumeona nguzo zimesimikwa na nyaya zimeanza kuwekwa kwenye nguzo, hivyo ameweza kutekeleza maelekezo.” Alisema
- Aliongeza kuwa, Mkandarasi huyo pia ameanza kazi ya kufunga transfoma kwa ajili ya kusambaza umeme kwa wananchi hivyo Bodi hiyo ilimtaka kuendelea kuongeza kasi ili maeneo yote muhimu pamoja na wananchi waunganishiwe umeme.
- Aidha, Bodi hiyo ilimwelekeza Mkandarasi huyo kuwasha umeme katika Kijiji cha Kakeneno na ifikapo mwishoni wa wiki ijayo wananchi wawe wameunganishwa na umeme kwani miundombinu imeshafika kijijini hapo na wananchi wameshafanya wiring kwenye nyumba zao.
- Vilevile, baada ya kukagua kazi ya usambazaji umeme katika Kijiji cha Mutundu, Bodi hiyo iliagiza umeme uwashwe tarehe 18 Novemba, 2019 kwani kuna miundombinu yote ya umeme na kilichobaki ni kuwasha tu umeme.
- Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kampuni Whitecity Guangdong JV, Nuhu Mringo alisema kuwa kampuni hiyo imejitahidi kutekeleza maagizo ya Bodi yaliyotolewa Wiki mbili zilizopita na kuahidi kuendelea kutekeleza kazi hiyo kwa kasi na kwa viwango.
- Ikiwa wilyani Chato, Bodi hiyo ilikagua kazi ya usambazaji umeme katika Kijiji cha Mutundu, Kakindo, Kamanga, Mnekez, Kakeneno na Matofali.Na Teresia Mhagama, Geita
Ad