RAIS MAGUFULI ATOA SHILINGI BILIONI 10 KWA AJILI YA UJENZI WA MAKAO MAKUU YA ULINZI WA TAIFA

  • Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametoa shilingi Bilioni 10 kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa katika eneo la Kikombo Jijini Dodoma.
  • Mhe. Rais Magufuli ametoa fedha hizo leo tarehe 25 Novemba, 2019 baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi huo na ameagiza milima yote inayozunguka eneo la Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa lenye ukubwa wa ekari 5,567 imilikiwe na JWTZ kwa ajili ya shughuli za ulinzi.
  • Kuhusu madai ya fidia, Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Bw. Godwin Kunambi kuwalipa fidia ya shilingi Bilioni 3 na Milioni 339 wananchi 1,500 wa Kata ya Kikombo ambao ardhi yao imechukuliwa na JWTZ kwa ajili ya Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa, kuanzia tarehe 01 Desemba, 2019.
  • Pamoja na agizo hilo, Mhe. Rais Magufuli amewatahadharisha wananchi wa Kikombo kujiepusha na matapeli wanaowahamasisha kudai fidia wasiyostahili kwa mujibu wa sheria ama kudai ardhi isiyo yao.
  • Mhe. Rais Magufuli pia ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kujenga kwa kiwango cha lami kilometa 18 za barabara inayounganisha Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa na barabara kuu ya Dodoma – Morogoro.
  • Aidha, Mhe. Rais Magufuli amekubali ombi la Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jen. Venance Salvatory Mabeyo aliyeomba Serikali ibebeba jukumu la kulipa deni la takribani shilingi Trilioni 1 ambalo JWTZ inadaiwa baada ya kujengewa nyumba 6,064 za makazi ya Askari katika maeneo mbalimbali nchini, badala ya Askari kukatwa posho zao ili kupata fedha za kulipia deni hilo kama ilivyowekwa katika mkataba wa ujenzi.
  • “Nakuhakikishia hakuna kukatwa Askari yeyote, hilo deni litabebwa na Serikali, kabla sijaja hapa nimeshamwelekeza Waziri wa Fedha na Katibu Mkuu, na nafikiri kesho au keshokutwa wataanza kulipia hilo deni ambalo limeanza kuiva, tutaanza kulipa Dola za Marekani zaidi ya Milioni 25 (sawa na shilingi Bilioni 56 na Milioni 948). Mkataba ni kweli ulikosewa, nafikiri ilikuwa ni mwaka 2012/13 lakini siwezi kukubali makosa ya namna hiyo yakafanyika katika kipindi changu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
  • Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Maafisa na Askari wa JWTZ kwa kazi nzuri ya kulinda mipaka ya nchi na kushiriki katika operesheni za kulinda amani katika Mataifa mbalimbali, majukumu ambayo yamelijengea heshima jeshi hilo na Tanzania.
  • Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jen. Venance Salvatory Mabeyo wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa maelekezo yake ya kujengwa Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa katika eneo la Kikombo ambayo yanajengwa na jeshi lenyewe.
  • Mapema kabla ya kuweka jiwe la msingi la mradi huo, Mhe. Rais Magufuli ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa uwanja wa maadhimisho ya kitaifa katika eneo la Chamwino.
  • Ujenzi wa uwanja huo utakamilika Januari 2020 ukiwa na uwezo wa kuchukua watu 5,000 kwa gharama ya shilingi Bilioni 2, na awamu ya pili itahusisha ujenzi wa ukumbi wa mikutano, jengo la watu mashuhuri na jengo la kupumzikia watu.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Chamwino, 25 Novemba, 2019

Ad
Ad

Unaweza kuangalia pia

LIVE: UZINDUZI WA MAJENGO YA OFISI YA MANISPAA NA MKUU WA WILAYA KIGAMBONI JIJINI DSM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 11, Febuari, …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.