RAIS MAGUFULI AAGIZA UPANUZI HOSPITALI YA WILAYA YA CHATO KUANZA MARA MOJA

  • Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewataka viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato Mkoani Geita kuanza mara moja upanuzi wa majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Chato kwa kuwa Serikali imeshatoa shilingi Bilioni 1 kwa ajili ya ujenzi huo.
  • Mhe. Rais Magufuli ambaye hakufurahishwa na taarifa za viongozi wa halmashauri hiyo kupoteza muda mwingi wakibishana juu ya upanuzi huo licha ya fedha za ujenzi kutolewa tangu mwezi Julai 2019, ameonya kuwa Serikali haiwezi kuvumilia kuona watu wakipata shida kwa uzembe wa viongozi wachache wa Halmashauri.
  • Amemuagiza Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato Bw. Eliud Mwaiteleke kuhakikisha ujenzi wa majengo hayo unafanyika na kwa gharama zinazostahili.
  • Aidha, Mhe. Rais Magufuli amemtaka Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo Dkt. Ligobeth Kalisa kuhakikisha mashine ya x-ray inafanya kazi muda wote na wananchi wanapatiwa huduma kwa wakati. Amesisitiza kuwa “sio sawa kwa Hospitali ya Wilaya kukosa huduma za x-ray, eti kwa sababu ya hakuna mikanda ya kupigia picha”.
  • Mhe. Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo tarehe 06 Desemba, 2019 aliwatembelea na kuwapa pole wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Chato akiwemo Mzee Zephania Petro Kanoge ambaye ndiye aliyemhamasisha kuingia katika siasa mwaka 1995.
  • Mzee Kanoge na mwenzake marehemu Constantine Misungwi walimfuata Mhe. Rais Magufuli mara mbili Jijini Mwanza alikokuwa akifanya kazi katika Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza wakimtaka agombee Ubunge, licha ya kukataa wazee hao waling’anga’ania hadi alipokubali na wakabeba jukumu la kumfanyia kampeni kwa kutumia pikipiki hadi aliposhinda Uchaguzi Mkuu.
  • Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mzee Kanoge kwa mchango wake mkubwa katika Maisha yake ya siasa na amemuombea apone haraka ili aweze kurejea nyumbani na kuungana na familia yake.
  • Akiwa hospitalini hapo, Mhe. Rais Magufuli amewaona wagonjwa wengine pamoja na wanawake na watoto waliofika kupata chanjo ambapo amewahakikishia kuwa Serikali imeanza kuchukua hatua madhubuti za kuboresha huduma za afya ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya na hospitali mpya kote nchini, na kuongeza bajeti ya dawa kutoka shilingi Bilioni 31 hadi kufikia shilingi Bilioni 270.
  • Mhe. Rais Magufuli pia amekwenda eneo la Ginnery ambako ametoa pole kwa familia ya Mzee Mariganya Nghwenge aliyefariki dunia juzi tarehe 04 Desemba, 2019. Mzee Marigana anakumbukwa kwa ukulima wake hodari ambapo mwaka 1967 alizalisha mihogo mingi ukiwemo mhogo mkubwa alioutumia kumuonesha Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere alipotembelea Chato na kuzungumza na wananchi.
  • Mjini Chato, Mhe. Rais Magufuli amewasalimu wananchi waliokuwa wamesimama kando mwa barabara, na waliokuwa wakiendelea na biashara zao madukani ambapo wananchi hao wamemuombea, wamempongeza kwa uongozi madhubuti ulioonesha mabadiliko makubwa katika kipindi kifupi na wamemtakia heri katika majukumu yake.
Ad

Unaweza kuangalia pia

LIVE: UZINDUZI WA MAJENGO YA OFISI YA MANISPAA NA MKUU WA WILAYA KIGAMBONI JIJINI DSM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 11, Febuari, …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *