- Mradi wa ujenzi wa kufua umeme wa maji (megawati 80) wa Rusumo, unaotekelezwa kwa ushirikiano wa nchi za Tanzania, Burundi na Rwanda, umefikia asilimia 59 kutoka 32 iliyokuwa imefikiwa Juni mwaka huu.
- Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti (aliyemaliza muda wake) wa Mawaziri wanaohusika na Mradi huo kutoka nchi husika, ambaye ni Waziri wa Nishati (Tanzania), Dkt Medard Kalemani, wakati akitoa mrejesho wa mkutano wa 11 wa Mawaziri hao kwa waandishi wa habari, uliofanyika Desemba 6, 2019 wilayani Ngara, mkoani Kagera.
- Waziri Kalemani alisema kuwa baada ya kufanya ukaguzi, yeyé na mawaziri wenzake wameridhishwa na maendeleo ya mradi husika, lakini wametoa maelekezo kadhaa kwa mkandarasi na timu ya wataalamu wanaosimamia mradi huo, ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati na viwango stahiki kama ilivyokusudiwa.
- “Tumeona kuna hali nzuri ya utekelezaji. Hata hivyo, tumetaka mkandarasi pamoja na wasimamizi wakamilishe kazi ndani ya muda uliopangwa ambao ni Februari, 2020.”
- Katika hatua nyingine, mawaziri hao wamekataa ombi la mkandarasi kuongezewa muda wa kukamilisha mradi huo ambapo aliomba akabidhi mradi Julai 2021 badala ya Februari mwakani.
- Akielezea sababu za mkandarasi kuomba kuongezewa muda, Waziri Kalemani alisema ni kutokana na malalamiko ya baadhi ya wananchi wanaoishi jirani na eneo unapotekelezwa mradi, ambao waliwasilisha malalamiko ya nyumba zao kuathiriwa na milipuko inayofanyika.
- “Kwa sababu hiyo, mkandarasi ameomba muda zaidi ili afanye tathmini kuhusu malalamiko hayo na ajipange kufanya milipuko isiyo na madhara kwa jamii. Hata hivyo, sisi tumekataa ombi lake na kumtaka akamilishe kazi ndani ya muda uliopangwa.”
- Akifafanua zaidi, Waziri alieleza kuwa, yeyé na mawaziri wenzake, wamemtaka mkandarasi kuwasilisha mapendekezo yanayoeleza bayana kwanini aongezewe muda ili wajiridhishe maana wao wanaamini kwa kutumia utaalamu wake, mkandarasi anaweza kutekeleza mradi huo kwa wakati huku akizingatia kufanya milipuko isiyo na madhara kwa wananchi.
- Akizungumzia suala la uwepo wataalamu wanaosimamia mradi husika, Dkt Kalemani alisema kuwa wameagiza ifikapo mwisho wa mwezi huu, timu ya wataalamu hao 12 wakiwemo wapya waliopatikana hivi karibuni; wahakikishe wanahamia kwenye nyumba zao zilizoko eneo la mradi ambazo mawaziri hao wamejiridhisha kuwa zimekamilika, baada ya kuzikagua.
- Mawaziri husika wamewataka wasimamizi hao wa mradi kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao ipasavyo kwa weledi na uaminifu ili ukamilike kwa wakati na viwango vinavyotakiwa.
- Vilevile, wameagiza mradi huo unaogharimu Dola za Marekani milioni 340 utekelezwe kwa mtindo wa kazi zote husika kwenda sambamba.
- Waziri Kalemani alizitaja kazi hizo kuwa ni pamoja na ujenzi wa mtambo wa uzalishaji, ujenzi wa bwawa, ujenzi wa njia za kusafirisha umeme kutoka eneo la mradi kupitia Nyakanazi (Tanzania) umbali wa kilomita 94, Rwanda (kilomita 161) na kutoka Rusumo hadi Burundi (kilomita 194).
- Awali, Waziri Kalemani alilazimika kusimama na kuzungumza na wananchi wa Rusumo ambao walikuwa na malalamiko ya kudai fidia ambapo aliagiza fidia zao zianze kulipwa mara moja kuanzia Desemba 15, mwaka huu.
- Aidha, aliagiza wananchi hao waletewe matenki ya kuhifadhia maji safi ili waondokane na adha ya kutumia maji yasiyo salama kutoka Mto Rusumo, ambayo walikuwa wakikabiliana nayo.
- Katika Mkutano huo wa 11 wa Mawaziri husika, Mwenyekiti anayemaliza muda wake, Dkt Medard Kalemani (Tanzania) alikabidhi nafasi hiyo kwa Mwenyekiti mpya ambaye ni Waziri wa Nishati na Migodi kutoka Burundi, Mhandisi Come Manirakiza.
Ad