GWAJIMA ASISITIZA UZALENDO, MAPITIO YA SERA YA UGATUAJI WA MADARAKA

  • Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Afya, OR-TAMISEMI Dkt. Dorothy Gwajima amewataka wakurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara zote kutanguliza uzalendo katika kufanya mapitio ya Sera ya Kitaifa ya Ugatuaji wa Madaraka.
  • Dkt. Gwajima ameyasema hayo mapema leo wakati wa kufungua kikao kazi cha Wakurugenzi wa Wizara zote wa Sera na Mipango  ambao wamekutana Jijini Dodoma kupitia Sera ya Taifa ya Ugatuaji wa Madaraka na Programmu ya kuimarisha Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
  • Dkt Gwajima amesema kuwa Wakurugenzi wote waliohudhuria kikao hiki ni wabobezi wa masuala ya mipango na bajeti katika Wizara zeo hivyo wanafahamu mahitaji ya wananchi halkadhalika mahitaji ya Wizara wanazofanyia kazi kwa upana wake kwahiyo wako katika nafasi nzuri ya kupitia Sera hii na kutoa mawazo yenye tija kwa manufaa ya Nchi yetu.
22-01
Naibu Waziri anyeshughulikia Afya OR-TAMISEMI Dkt. Dorothy Gwajima (aliyesimama) akifungua kikao kazi cha Wakurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara zote kupitia Sera ya Taifa ya Ugatuaji wa Madaraka kwa Wananchi.
  • “Kazi hii ni nyeti sana kwa mustakabali wa Taifa letu, mnatakiwa mjitoe kwa dhati na muweke uzalendo mbele ili kulinda maslahi ya Nchi yetu, mjitume haswa katika kufanya kazi hii kwa weledi na moyo wote kwa sababu ninyi ndio wataalamu katika eneo hili; Makundi mengine yamepitia Sera hii lakini ninyi ni wataalamu na wabobezi wa Sera hivyo mchango wenu wenye ni muhimu sana kwa mafanikio ya Sera hii” alisisitiza Dkt. Gwajima.
  • Akizungumzia mafanikio ya Sera iliyokwisha muda wake Gwajima amesema Sera hiyo ilisaidia katika ongezeko la uelewa na ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo na utawala, iliongeza ari ya Wananchi katika kujitegemea kupitia upangaji wa Mipango na kuimarika kwa taratibu za kuwajibisha watumishi na viongozi katika ngazi husika.
  • Gwajima aliongeza kuwa Sera hii pia ilisaidia kuboresha utoaji wa huduma ikiwemo Elimu, Afya, Maji, Miundombinu, biashara, makazi na ustawi wa jamii pamoja na kuimarika kwa uwajibikaji wa watumishi kwa kuwa wanasimamiwa katika ngazi ya msingi.
33-01
Baadhi ya Wakurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara wakifuatilia ufunguzi wa kikao kazi cha kupitia Sera ya Taifa ya Ugatuaji wa Madaraka kwa Wananchi kilichofanyika Jijini Dodoma mapema.
  • Wakati huo huo Gwajima alibanaisha changamoto za Sera hiyo kuwa ni pamoja na kuwepo kwa mitazamo inayokinzana kati ya watendaji na viongozi wa kisiasa katika ngazi za vijiji, Kata na halmashauri katika kuweka vipaumbele na kutekeleza miradi ya maendeleo na Mamlaka za Serikali za Mitaa kutegemea fedha kwa kiasi kikubwa kutoka Serikali Kuu.
  • Aliongeza kuwa Wizara za kisekta kutopeleka fedha zinazoendana na majukumu yaliyogatuliwa, mfumo hafifu wa mawasiliano kwa baadhi ya Wizara za Kisekta na OR-TAMISEMI pamoja kuwepo kwa Sera ya Ugatuaji iliyojengwa kwenye mfumo wa kisheria inayoelekeza mipaka, majukumu na utaratibu wa utekelezaji wake.
  • Naye Mkurugenzi wa Uratibu wa Sekta OR-TAMISEMI Dr. Andrew Komba amesema kuwa Sera iliyopo sasa ni ya mwaka 1998 hivyo imekwisha muda wake na kuna kila sababu ya kufanya mapitio ya Sera hiyo ili kuendana na mahitaji ya sasa na mabadiliko yaliyopo sasa.
  • “Tumehakikisha kuwa Sera ya sasa imefanyia kazi changamoto zote zilizojitokeza katika utekelezaji wa Sera iliyokwisha muda wake na itajikita zaidi katika ujenzi wa uchumi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kujenga uchumi wa jamii na pia imejikita katika ushirikishwaji wa sekta binafsi pamoja na asasi zisizo za Kiserikali katika kutoa huduma bora kwa jamii.
  • Kwa kuwa sasa tunaelekea katika Uchumi wa Viwanda tumehakikisha Sera hii inajielekeza katika ushiriki kikamilifu katika ujenzi wa viwanda na inalenga maridhino ya makundi yote yaani Serikali, Sekta binafsi, Asasi zisizo za kiserikali, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa” alisisitiza Dr. Komba
  • Kikao hiki cha siku mbili kitapitia na kujadili rasimu ya Sera ya Ugatuaji wa madaraka kwa wananchi, mkakati wa utekelezaji wa Sera pamoja na Programu ya kuimarisha Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI
Ad

Unaweza kuangalia pia

RAIS MAGUFULI AIPONGEZA MAHAKAMA NA WADAU KWA MAFANIKIO MAKUBWA

Rais  Dkt. John  Magufuli ameipongeza Mahakama na wadau wake kwa hatua kubwa za kimaendeleo zilizopigwa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *