- Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ametoa siku 23 pekee kwa wakandarasi wanaojenga Skimu ya Umwagiliaji ya Nanganga wilayani Ruangwa kuwa wamekamilisha ujenzi wa mradi huo.
- Waziri Hasunga ametoa agizo hilo leo tarehe 12 Disemba 2019 la kukamilika kwa mradi huo wakati alipotembelea na kukagua skimu hiyo yenye hekta zipatazo 300 akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Lindi.
- Amesema kuwa mradi huo unaohusisha ujenzi wa banio katika mto Lukuredi, mfereji mkuu wenye urefu upatao mita 525, mfereji wa kati wenye urefu upatao mita 2675, mifereji midogo vigawa maji pamoja na vivuko vya miguu ulipaswa kukamilika Julai 2, 2019 lakini mpaka sasa umeshindwa kukamilika kwa wakati jambo ambalo limewakosesha wakulima fursa ya kilimo cha umwagiliaji.
- “Mkandarasi aliomba aongezwe muda wa miezi mitano baadaye ameongezwa tena mwezi mmoja lakini mpaka sasa ameshindwa kukamilisha nadhani ameamua kutuchezea akili hatutakubaliana na hilo hata kidogo” Alikaririwa Mhe Hasunga
- Akizungumza na wananchi wa Kijiji na kata ya Namanga Mhe Hasunga amesema kuwa miradi mingi ya umwagiliaji nchini haikamiliki kwa wakati kutokana na wakandarasi kutotekeleza majukumu yao ipasavyo.
- “Haiewezekani Waziri Mkuu anayechapa kazi, anahangaika nchi nzima kila kona halafu kwake ndio mradi uwe haujakamilika hivi tutakuwa na akili timamu kweli hilo halikubaliki” Alisema
- Amemtaka mkandarasi kuhakikisha kuwa mradi huo unakamilika ndani ya muda uliokubaliwa vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
- Waziri Hasunga amesema kuwa serikali inajipanga na mkakati kabambe wa kuhakikisha kuwa hakutaanzishwa miradi mipya ya umwagiliaji mpaka pale miradi iliyoanzishwa itakapokuwa imekalmilika.
- Kuna miradi mingi imeanzishwa lakini haijakamilika ilihali kiasi kikubwa cha fedha kinakuwa kimetumika.
- Mradi wa umwagiliaji Nanganga ni kati ya miradi 16 ya SSIDP III (Small Scale Irrigation Development Project) awamu ya tatu iliyojengwa na serikali ya Tanzania chini ya wizara ya Kilimo na kusimamiwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC).
- Katika ziara hiyo ya kikazi Waziri Hasunga ametembelea na kukagua skimu ya umwagiliaji Narunyu katika Halmashauri ya Mtama yenye eneo la hekta 1200 zinazofaa kwa umwagiliaji.
- Vilevile Waziri Hasunga ametembelea na kukagua ghala la kuhifadhia korosho la BUKO kadhalika ghala la kuhifadhia korosho la Mtama ambapo amepongeza utunzaji wa korosho za wakulima katika maghala hayo.Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo- Lindi
Ad