- Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imetumia zaidi ya shilingi bilioni 1.2 kwa mwaka 2019 kwa ajili ya kulipa gharama za matibabu ya moyo kwa wagonjwa wanaotoka katika familia maskini na wasiokuwa na uwezo wa kulipia gharama hizo.
- Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Agnes Kuhenga wakati akizungumza na waandishi wa Habari mara baada ya kupokea msaada wa vifaa tiba pamoja na dawa kutoka Ubalozi wa China kupitia Timu ya madaktari kutoka nchini humo wanaofanya kazi hapa nchini.
- Agnes ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Utawala na Fedha alisema asilimia 10 hadi 15 ya wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo hawana kadi za bima ya afya na hawana uwezo wa kulipia gharama za matibabu. Wagonjwa wa aina hiyo wanapata huduma za matibabu kwa Taasisi kugharamia matibabu yao.
- “Januari mwaka huu hadi siku hii ya tarehe 19/12/2019 tumetumia zaidi ya shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya matibabu ya wagonjwa ambao hawakuwa na uwezo wa kuchangia gharama za matibabu. Ninaiomba mifuko ya bima za afya iweze kutoa elimu kwa watanzania ili wajiunge na bima hizo ambazo zitawapunguzia wananchi gharama ya kulipia fedha za matibabu pindi watakapougua”, alisema Agnes.
- Akizungumzia kuhusu msaada huo Agnes aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya watu wa China kwa misaada mbalimbali ya huduma za afya wanayoitoa katika Taasisi hiyo na kwa upande wa vifaa tiba pamoja na dawa walizozitoa alisema zitatumika kwa wagonjwa wasiokuwa na uwezo wa kuchangia gharama za matibabu.
- Kwa upande wake mwakilishi wa Balozi wa Jamhuri ya watu wa China hapa nchini Yuan Lin alisema msaada wa vifaa tiba pamoja na dawa walizozitoa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kupitia madaktari wa Kichina wanaofanya kazi hapa nchini unathamani ya shilingi milioni 15.
- “Ninaamini msaada huu ambao ni moja ya kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na China katika sekta ya afya utasaidia katika matumizi ya kila siku ya Hospitali na utachangia katika kutoa huduma ya matibabu kwa wagonjwa”, alisema Lin.
Ad