- Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, amefungua kiwanda cha Nguzo cha Qwihaya, kilichopo katika Mtaa wa Kasanga, Wilaya ya Kasulu, Mkoani Kigoma
- Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara, mara baada ya ufunguzi wa kiwanda hicho Dkt. Kalemani alieleza kuwa Serikali ilikuwa inapata gharama kubwa kutoa Nguzo katika Mikoa mengine kuzifikisha Mkoani humo kabla ya kiwanda hicho kujengwa Mkoani humo.
- Alisema, maeneo ambayo yapo karibu na kiwanda hicho yatafikiwa na umeme kwa haraka kwasababu hakutakuwa na sababu ya ucheleweshaji wa kupeleka umeme katika maeneo hayo ambayo, kiwanda cha nguzo kipo karibu.
- Aliongeza kuwa, Serikali haitakubali kuona ucheleweshwaji wa usambazaji umeme vijijini, kupitia TANESCO au Wakandarasi, kwasababu ya uwepo wa kiwanda hicho Mkoani humo umewarahisishia kazi na bei ya nguzo itashuka ikilinganishwa na bei ya Nguzo ambazo zinatoka katika Mikoa ya Njombe na Iringa.
- “ Maelekezo yangu kwa TANESCO ni kuanza kuzichukua nguzo hizi kwa njia ya ushindani hakuna tena sababu ya kusema nguzo hakuna na nataka kazi zimalizike ndani ya muda kwasabau vitendea kazi vipo na pesa ipo” alisema.
- Alifafanua kuwa, mahitaji ya nguzo kwa sasa nchini ni milioni moja na nusu kwa mwaka lakini wazalishaji nchini wanauwezo wa kuzalisha zaidi ya nguzo milioni tatu ukilinganisha na mwaka 2015 ambapo mahitaji ya nguzo yalikuwa milioni moja na nusu lakini nguzo zilizokuwa zinapatikana nchini ni laki nne tu, ambapo nguzo nyingi zilikuwa zinatoka Nchi za nje lakini kwa uwepo wa viwanda nchini imesaidia sana upatikanaji wa nguzo kwa wingi.
- Alieleza kuwa, kwa kipindi cha miaka minne viwanda vya nguzo tisa vimejengwa nchini, mara baada ya Serikali kupiga marufuku ya ununuaji nguzo kutoka nchi za nje ambao ulikuwa unachelewesha usambazaji wa umeme nchini .
- Aidha, alimpongeza muwekezaji wa kiwanda hicho, kwa kujitolea kujenga kiwanda kwenye eneo hilo pamoja na kumiliki viwanda vyengine Mkoani Njombe na Iringa na kuamua kuwekeza katika maeneo mengine ya nchini.
- Kwa kuona umuhimu wa Viwanda hivyo, Waziri Kalemani ametoa wito kwa wawekezaji wengine wajitokeze kujenga viwanda vya Nguzo, katika Mikoa mengine nje ya Mkoa wa Iringa na Njombe ili kutimiza azma ya Rais ya Tanzania ya Viwanda.
- Awali, Kaimu Mkurugenzi wa kiwanda hicho Beruto Kaboda ameleza kuwa kiwanda chao kimeamua kimeitikia wito wa Rais, wa Tanzania ya Viwanda kwa vitendo kwa kuchukua hatua ya kujenga kiwanda hicho chenye uwezo wa kuzalisha zaidi ya nguzo laki moja kwa mwaka.
- Vile vile, alieleza kuwa kwasasa soko lao kubwa lipo hapa nchini na mteja wako mkubwa ni Shirika la Umeme Tanzania( TANESCO) ambapo kipindi hiki cha utekelezaji wa mradi wa REA awamu ya tatu soko la nguzo limekuwa kubwa na kuwalazimu kufanya kazi kwa masaa 24.
- Pia alitoa shukrani zake kwa Waziri wa Nishati Dr Medard Kalemani na Naibu Waziri Subira Mgalu kwa kuwasimamia wazalishaji wa nguzo nchini na kutoa miongozo ambayo inawapa hamasa ya kufanya kwa bidii na kuhakikisha wanazalisha nguzo bora na zinawafikia wananchi wa vijiji kwa haraka zaidi.
- Hafsa Omar-Kigoma
Ad