Na Said Mwishehe, Michuzi Globu ya jamii
- Imeelezwa kuwa Bandari ya Kiwira ni lango kuu la usafirishaji wa mizigo katika Ziwa Nyasa ambapo asilimia zaidi ya 90 ya shehena zinazohudumiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania(TPA) katika ziwa hilo hupitia katika bandari hiyo.
- Hayo yameelezwa na Meneja wa Bandazi za Ziwa Nyasa Abedi Gallus wakati akizungmza na waandishi wa habari katika mahojiano maalumu kuhusu bandari za ziwa hilo tangu Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani ambapo pamoja na mambo mengine imeweka mkazo wa kuhakikisha usafiri wa bandari katika maziwa makuu unaimarika.
- Amesema bandari ya Kiwira ni muhimu katika upitishaji wa makaa ya mawe kutoka katika Wilaya ya Nyasa na Mbinga zilizopo mkoani Ruvuma , pia bandari hiyo inatumika kuhudumia mizigo mchanganyiko inayosafirishwa kwa njia ya maji katika ukanda wote wa Ziwa Nyasa.
- Amesema kwa kuzingatia umuhimu wa bandari hiyo Serikali ya Awamu ya Tano kwa kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari katika mwaka wa fedha wa 2018/2019 inatekeleza miradi miwili muhimu ya upanuzi bandari ya Kiwira ili kuboresha ufanisi wa kazi za bandari hiyo.
- Amesema hivyo katika bandari hiyo kuna mradi wa ujenzi wa sakafu ngumu, ambapo utagharimu jumla ya fedha Sh.bilioni 2.45 zinazotokana na mapato ya ndani ya mamlaka hiyo na kwamba mradi huo ni wa miezi tisa na unatekelezwa na mkandarasi Pioneer Builders Ltd kutoka Dar es Salaam.”Mradi huu upo katika hatua za mwisho kukamilika na sasa umekamilika kwa asilimia 85.”
- Gallus amesema lengo kuu na mradi huo ni kupanua wigo wa kuhifadhi shehena hususan ya makaa ya mawe ambayo yatakuwa yakisafirishwa kwa wingi mpaka bandari ya Kiwira na kuchukuliwa na malori kwa ajili ya kusambazwa kwa wateja.Aidha ujenzi huo utaiwezesha bandari hiyo kuhudumia shehena nyingi zaidi kwa wakati mmoja na kuboresha mzunguko wa meli kwani mzigo wote unaowasili na meli utakuwa ukipakuliwa kwenye yadi na kuruhusu meli kwenda kuchukua mzigo mwingine.
- Pia kuna ujenzi wa gati mbili kwa ajili ya kufunga meli, jengo la ofisi na mgahawa ambapo Gallus amesema mradi wa ujenzi wa gati hizo, jengo la ofisi na mgahawa katika bandari ya Kiwira utagharimu jumla ya fedha Sh.bilioni 1.257 zinazotokana na mapato ya ndani mamlaka hiyo.”Mradi huu ni wa miezi 12 na unatekelezwa na mkandari Summer Communication Co.Ltd kutoka Njombe.Mradi huu umefikia asilimia 90 na unatarajiwa kukamilika Januari mwaka 2020.”
- Amesema kuwa kuu la mradi huo ni kuongeza ufanisi wa bandari ya Kiwira kwa kuiwezesha kuhudumia idadi kubwa ya meli kwa muda mchache.Aidha kukamilika kwa mradi huo utaiwezesha bandari ya Kiwira kuhudumia meli tatu kwa wakati mmoja tofauti na hakutakuwa na ucheleweshaji wa meli unaotokana na kusubiri nafasi ya kufunga gati.
Ad