- Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein ametunuku Nishani ya Mapinduzi, Nishani ya Utumishi Uliotukuka pamoja na Nishani ya Ushujaa kwa Viongozi, Watumishi wa Umma, Maafisa na Wapiganaji wa Idara Maalum za SMZ na wananchi mbali mbali wenye sifa maalum.
- Hafla hiyo ilifanyika katika viwanja vya Ikulu jijini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Serikali, Vyama vya siasa, viongozi wakuu wastaafu akiwemo Rais Mstaafu wa Awamu ya Sita wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dk. Amani Abeid Karume, Makamo wa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohamed Kharib Bilal.
- Viongozi wengine waliohudhuria ni Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, Waziri Kiongozi Mstaafu Shamsi Vuai Nahodha, Mawaziri na viongozi wengine wa Serikali, wananchi na wanafamilia, hafla ambayo ni muendelelezo wa shamra shamra za miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964.
- Mapema akitoa tamko la Kwanza la kuashiria kuanza shughuli hiyo, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Salum Maulid Salum alisema kuwa Rais Dk. Shein ametunuku Nishani 37 ya Mapinduzi, Nishani 10 ya Utumishi Uliotukuka na Nishani 25 ya Ushujaa kwa Viongozi, Watumishi wa Umma, Maafisa na Wapiganaji wa Idara Maalum za SMZ pamoja na wananchi mbali mbali.
- Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa sherehe hiyo ilihudhuriwa na watunukiwa 72 ambao kati ya hao 22 ni Marehemu ambao Nishani zao zimepokelewa na wawakilishi wao na 50 wako hai ambapo nishani zao watapokea wenyewe au zitapokewa kwa niaba yao.
- Alisema kuwa Watunuku wote sifa zao zimekidhi matakwa ya Nishani hizo ambapo Nishani ya Mapinduzi hutolewa kwa mtu ambaye aliasisi au alishiriki au aliyatukuza na aliyaenzi Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964.
Ad