Rais Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 27 Januari, 2020 amewaapisha Mawaziri 2 na Mabalozi 3 aliowateua hivi Karibuni.
Mawaziri walioapishwa ni George Boniface Mwataguluvala Simbachawene aliyeapishwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mussa Azzan Zungu aliyeapishwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.
Mabalozi walioapishwa ni Mhe. Maimuna Kibenga Tarishi aliyeapishwa kuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Geneva – Uswisi, Hussein Athuman Kattanga aliyeapishwa kuwa Balozi wa Tanzania Tokyo – Japan na Prof. Kennedy Godfrey Gastorn aliyeapishwa kuwa Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa New York Marekani.
Akizungumza baada ya kuwaapisha na kushuhudia wakila kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma, Rais Magufuli amewataka viongozi hao kwenda kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, uchapakazi, kutanguliza maslahi ya Tanzania pamoja na kushirikiana vizuri na viongozi na watendaji wengine katika wizara zao.
Amemtaka Mhe. Waziri Simbachawene kushughulikia dosari zilizopo katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ikiwemo kuhakikisha watendaji na viongozi ambao ni kikwazo katika ufanisi wa wizara wanaondolewa, pamoja na kushughulikia makubaliano yaliyotiwa saini na viongozi wakuu wa wizara waliopita kuhusu mkataba wa ununuzi wa vifaa vya zimamoto (vyenye thamani ya zaidi ya shilingi Trilioni 1) katika mazingira yasiyokuwa na uadilifu na bila kujali maslahi ya Taifa.
Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na imehudhuriwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu na Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama.