SERIKALI YAJIZATITI KUIMARISHA USIMAMIZI NA UDHIBITI WA RASILIMALI MADINI

  • Serikali imedhamiria kuwa na mikakati endelevu ya kusimamia na kudhibiti rasilimali madini ili ilete tija iliyokusudiwa kwa Taifa.
  • Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (Mb) leo Januari 25, 2020 Jijini Dodoma alipokuwa akifungua kikao kazi cha siku mbili kwa Vyombo vya Ulinzi na Usalama kuhusu usimamizi na udhibiti wa rasilimali madini.
5-01
Katibu Mkuu Wizara ya Madini Prof. Saimon Msanjila akieleza jambo wakati wa Kikao kazi hicho.
  • Waziri Mhagama alieleza kuwa, Serikali imekua ikichukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha kunakuwa na usimamizi na udhibiti wa rasilimali madini ikiwemo maboresho Sheria ya Madini ya mwaka 2010 pamoja na Marekebisho yake yote, Kanuni  na taratibu  zilizotolewa na Mamlaka husika ili kuchochea ukuaji wa sekta hiyo katika kuchangia pato la Taifa.
  • “Kuna umuhimu mkubwa kushirikisha Vyombo vya Ulinzi na Usalama katika mchakato huu ili rasilimali hii ya madini iweze kusimamiwa vyema, Sambamba na kuwa na mifumo mizuri ambayo itaimarisha usimamizi wa sekta hiyo, hivyo ni vyema kukawa na ushirikiano wa kutosha ili sekta ya madini iwe endelevu katika kukuza uchumi wa nchi,” alisisitiza Mhagama
2-01
Sehemu ya Wawakilishi kutoka kwenye Vyombo vya Ulinzi na Usalama wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi hicho.
  • Alieleza kuwa, Sekta ya Madini hapo awali ilikuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na utoroshwaji wa Madini kwenda nchi za nje bila kulipiwa tozo zinazotakiwa, ukwepaji wa kodi stahiki na mambo mengine mengi ambayo ni kinyume na Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo.
  • “Natumaini kupitia Semina hii mtakuwa na uelewa wa Sekta ya Madini na hivyo kuwa na mikakati mizuri ya usimamizi na udhibiti thabiti utakaopelekea Sekta kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa,” alisema Mhagama
3-01
Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko (kulia) na Kamishna wa Utawala na Rasilimali Watu wa Jeshi la Polisi, Benedict Wakulyamba wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi hicho.
  • Aliongeza kuwa, Serikali imefanikiwa pia kufungamanisha Sekta ya Madini na maendeleo ya Wananchi kwa kuwaleta pamoja, wawekezaji katika sekta hiyo wameweza kujitolea kwenye huduma mbalimbali za kijamii kama vile masula ya afya, elimu, maji n.k akitolea mfano Mgodi wa Geita ambao umekuwa ukitoa wastani wa Shilingi Bilioni 10 kwa mwaka kwa ajili ya kusaidia huduma za kijamii.
  • “Pongezi nyingi zimwendee Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kuleta mageuzi katika sekta ya Madini,” alisisitiza Mhagama.
4-01
Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko akifafanua jambo wakati wa Kikao Kazi hicho kilichohusisha Vyombo vya Ulinzi na Usalama ili kuwajengea uelewa wa Sekta ya Madini.
  • Aidha, Waziri Mhagama amezitaka Idara na Taasisi zilizoshiriki kikao Kazi hiko zitambue wajibu wao katika kukuza Sekta ya Madini nchini na kutoa msaada wa kiufundi pindi unapohitajika bila kuathiri shughuli za sekta hiyo na masuala ya uwekezaji.
  • Pamoja na hayo, amelitaka Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) kuhakikisha wanakuwa na Mwongozo utakaokuwa unawashirikisha kikamilifu Watanzania katika miradi ya kimkakati katika shughuli za mbalimbali za kiuchumi nchini ikiwemo Sekta hiyo ya Madini, Gesi, Mafuta,Viwanda, Ujenzi na Utalii na Kilimo.
  • Kwa Upande wake Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko alieleza kuwa Serikali imeleta mageuzi makubwa katika Sekta ya Madini ikiwemo uanzishwaji wa Masoko ya Madini sehemu mbalimbali za Mikoa nchini ambayo yamesaidia sana uwepo wa mifumo rasmi ya mapato ya madini na kupunguza utoroshwaji wa madini.
6-01
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto (kulia) akiwa pamoja na Makamanda wa Polisi kutoka mikoa mingine wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa kwenye kikao kazi hicho.
  • “Kwa mwaka wa fedha 2019/20 Serikali imeweza kukusanya jumla ya Shilingi Bilioni 242 ikiwa ni sawa na asilimia 103, mafanikio hayo yametokana na uwepo wa ushirikiano wa wadau wa sekta hiyo katika kuhakikisha inasonga mbele,” alisema Biteko
  • Naye Kamishna wa Utawala na Rasilimali Watu wa Jeshi la Polisi, Benedict Wakulyamba akizungumza kwa niaba ya Jeshi la Polisi alisema wapo tayari kutoa ushirikiano wakati wowote ili rasilimali za Taifa ziweze kuwa kwenye usalama wakati wote.
  • “Tutaungana kwa pamoja kama vyombo vya ulinzi na usalama ili tuweze kusimamia rasilimali za taifa kwa pamoja,” alieleza Wakulyamba
  • Kikao Kazi hicho cha siku mbili kimehusisha Vyombo vya Ulinzi na Usalama kutoka Makao Makuu na katika Mikoa yote hapa nchini.
Ad

Unaweza kuangalia pia

UCHUMI WA TANZANIA WAZIDI KUKUA NA KUIMARIKA

Hali ya uchumi wa Tanzania yazidi kuimarika na kukua  kwa asilimia 6.9 ikiwa ni  takwimu …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *