BALOZI WA ISRAEL ATEMBELEA TAASISI YA MOYO JAKAYA KIKWETE (JKCI)

  • Israel imeahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania kupitia Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kuhakikisha watoto wenye magonjwa ya moyo wanapata matibabu kwa wakati.
  • Hayo yamesemwa jana na Balozi wa nchi hiyo nchini mwenye makazi yake Jijini Nairobi nchini Kenya Mhe. Oded Joseph alipotembelea Taasisi hiyo kwa ajili ya kuona huduma mbalimbali za matibabu ya moyo zinazotolewa.
1-01
Daktari wa watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Amanda Anyoti akimwelezea balozi wa Israel nchini mwenye makazi yake jijini Nairobi nchini Kenya Mhe. Oded Joseph jinsi wanavyowahudumia watoto wenye matatizo ya moyo wakati balozi huyu alipotembelea JKCI jana kwa ajili ya kuona huduma mbalimbali za matibabu ya moyo zinazotolewa.
  • Balozi Oded aliipongeza Taasisi hiyo kwa kutoa matibabu ya moyo ya kibingwa ambayo yamesaidia kuokoa maisha ya wagonjwa.
  • “Shirika la Save a Child’s Heart (SACH) la nchini Israel limekuwa likishirikiana na Taasisi hii kwa kufanya matibabu ya pamoja kwa watoto wenye matatizo ya moyo. Watoto ambao wamekutwa na matatizo yanayohitaji matibabu ya hali ya juu wamekuwa wakipelekwa nchini Israel kwa ajili ya matibabu hayo na gharama za matibabu zinagharamiwa na SACH”, alisema Mhe. Balozi Oded.
3-01
Daktari bingwa wa usingizi na wagonjwa walioko katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Faraji Lydenge akimsomea balozi wa Israel nchini mwenye makazi yake jijini Nairobi nchini Kenya Mhe. Oded Joseph taarifa ya mtoto anayefanyiwa upasuaji mkubwa wa kusimamisha moyo na kuzibwa tundu la moyo wakati balozi huyo alipotembelea chumba cha upasuaji. Mhe. Balozi Joseph alitembelea Taasisi hiyo jana kwa ajili ya kuona huduma mbalimbali za matibabu ya moyo zinazotolewa.
  •  “Nimetembelea maeneo mbalimbali ya Taasisi nimeona kazi nzuri mnayoifanya hakika mnahitaji pongezi kwa kuokoa maisha ya watu walio katika hatari ya kupoteza uhai wao kutokana na magonjwa haya ya moyo, Israel itaendelea kushirikiana nanyi kurudisha furaha ya watoto hawa” alisema Mhe. Balozi Oded
  • Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi ameishukuru Serikali ya Israel kupitia Shirika la Save a Child’s Heart (SACH) kwa kuendelea kuwajengea uwezo wataalamu wa Taasisi hiyo  na kuwawezesha kupata mbinu mpya za kitabibu zinazoendana na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
  • Aidha Prof. Janabi amemuomba balozi huyo kuangalia namna ambavyo Israel itaiwezesha JKCI kuwa na jengo maalum na lenye mahitaji yote ya watoto wenye magonjwa ya moyo ili watoto wanaosubiri kwenda nchini Israel kwa ajili ya matibabu waweze kuishi katika mazingira ya karibu na Taasisi.
4-01
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akizungumza na Balozi wa Israel nchini mwenye makazi yake jijini Nairobi nchini Kenya Mhe. Oded Joseph alipotembelea taasisi hiyo jana Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuona huduma mbalimbali za matibabu ya moyo zinazotolewa. Picha na: JKCI
  • “Tungeweza kupata jengo ambalo tungekuwa tunawaweka watoto wetu wanaosubiria kwenda nchini Israel kwa ajili ya matibabu ya moyo kama ilivyo Israel wanavyowekwa kwenye jengo maalamu lenye mahitaji yote itasaidia kuwasimamia kwa ukaribu zaidi na kuwasafirisha pale inapohitajika tofauti na ilivyo sasa inatuchukua muda kuwakusanya kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania” alisema Prof. Janabi
  • Kuwepo kwa jengo hilo la kuwahifadhi watoto kwa ajili ya maandalizi ya kwenda nchini Israel litapunguza muda wa kuwatafuta watoto hao kutoka vijijini kwa ajili ya safari ya Israel lakini pia watoto watakuwa wanapata huduma za matibabu mara kwa mara hivyo kupunguza maambukizi mengine yanayoweza kuyapata wanapokuwa nje ya mazingira ya Hospitali.
  • Tangu mwaka 2015 Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete imekuwa ikishirikiana na Israel kupitia taasisi ya Save a Child’s Heart kwa kufanya matibabu ya pamoja,  kuleta vifaa vya matibabu pamoja na kuwapeleka watoto wenye magonjwa ya moyo yanayohitaji utaalamu wa hali ya juu kutibiwa nchini humo. Hadi sasa watoto 75 wameshatibiwa nchini Israel na hali zao zinaendelea vizuri.
Ad

Unaweza kuangalia pia

ONGEZENI KASI YA KUWAHUDUMIA WANANCHI – DKT. CHAULA

Watumishi wa afya nchini wametakiwa kuongeza kasi ya kuwahudumia wananchi kwenye vituo vya kutolea huduma …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *