SERIKALI KUJENGA DAMPO LA KISASA JIJINI DAR ES SALAAM

  • Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu amesema Serikali inatarajia kujenga dampo la kisasa katika Mkoa wa Dar es Salaam ili liweze kuhimili taka zote zinazozalishwa mkoani humo.
  • Zungu amesema hayo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Kawe Halima Mdee aliyeuliza kuwa Serikali ina mkakati gani wa kujenga madampo mengine katika wilaya zote za mkoa huo kwani hivi sasa kuna dampo moja la Pugu Kinyamwezi.
1a-01
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu akitoa ufafanuzi wa swali la nyongeza lililoulizwa bungeni jijini Dodoma leo na Mbunge wa Kawe Mhe. Halima Mdee kuhusu mikakati ya Serikali kujenga madampo mengine ili kukidhi mahitaji ya Jiji la Dar es Salaam.
  • Alibainisha kuwa kiasi cha sh. bilioni 75 zimetolewa na wafadhili kwa ajili ya kazi hiyo ambayo itakwenda sambamba na ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami katika eneo la dampo ili kurahisha usafirishaji wa taka ambapo Halmashauri ya Jiji hilo imetenga fedha.
  • “Kasi ya taka zinazozalishwa Dar es Salaam ni kubwa na jiji linakua kwa asilimia kubwa sana na kwa miaka miwili ijayo kasi ya population itafika milioni 8 hadi 9 na dampo ni moja na juzi mimi nimetembelea, dampo hali ya dampo ni mbaya lazima tukiri ni mbaya miundombinu ni mbaya hatua zimeshachukuliwa,” alisema Zungu.
  • Awali akijibu maswali ya msingi ya Mbunge Mdee kuhusu mkakati gani wa Serikali wa kukabiliana na tatizo la uchimbaji mchanga na uchafuzi uliokithiri jijini humo, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima alisema ni kweli uchimbaji huu huleta athari ikiwa ni pamoja na mmomonyoko wa kingo za mito, uharibifu wa maji na miundombinu na mwingiliano wa maji ya bahari katika nchi kavu.
1b-01
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima akijibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa na wabunge Daniel Nswanzugwako (Kasuliu Mjini) na Halima Mdee (Kawe) wakati wa kipindi cha maswali na majibu mapema leo bungeni jijini Dodoma.
  • Alitaja zingine kuwa ni kubadilika kwa mkondo wa mto kutoka uelekeo wa asili, kuharibika kwa uimara wa mto, uharibifu wa mimea ya asili ambayo husaidia kupunguza mmomonyoko na uharibifu wa mazalia ya viumbe hasa wakati kina cha maji kinapoongezeka.
  • Hivyo alibainisha kutokana na changamoto hizo aliweka wazi kuwa Serikali inaandaa mkakati wa muda mrefu unaotokana na mapendekeo ya Kamati Maalum ya wadau iliyoundwa na Ofisi hiyo kupendekeza hatua za kuchukuliwa ili kuwa na uchimbaji endelevu wa mchanga na usiokiuka Sheria za nchi.
  • Aliongeza kuwa zitafanyika tafiti na kuendeleza teknolojia za ujenzi zinazoweza kutumia mchanga kidogo na kuelimisha wananchi kuhusu athari za uchimbaji holela wa mchanga na kuzuia uchimbaji holela.
1n-01
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu (kushoto) akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza  John Mongella katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma leo. Katikati ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima
  • Aidha, Sima alisema kuwa mamlaka mbalimbali zikiwemo Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Mamlaka za Mabonde na Tume ya Madini kupitia Ofisi ya Madini Mkoa wa Dar es Salaam, zimekuwa zikifanya ukaguzi wa mara kwa mara na hatua stahiki kwa mujibu wa sheria huchukuliwa,
  • “Kuhusu uchafuzi wa mazingira uliokithiri, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 Kifungu 139(1) imetoa mamlaka kwa Serikali za Mitaa kuzuia au kupunguza taka ngumu, taka vimiminika, gesi taka na taka zenye madhara. Serikali itaendelea kuelimisha wananchi na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria,” alisisitiza Sima.
  • Aliongeza kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia programu ya Elimu kwa Umma inatoa elimu kuhusu usimamizi na udhibiti wa taka kuanzia ngazi ya jamii, viongozi na wadau, hasa katika eneo la urejelezaji wa taka ngumu na kutoa wito kwa Serikali za Mitaa kuwajibika kwa kuweka mipango endelevu ya usimamizi wa taka kama ilivyobainishwa katika Kifungu 139(1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004.

 

 

Ad

Unaweza kuangalia pia

WAZIRI ZUNGU AHUDHURIA MKUTANO WA 7 WA BARAZA LA KISEKTA LA MAWAZIRI WA MAZINGIRA NA MALIASILI WA JUMUIA YA AFRIKA MASHARIKI

             

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *