Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wazazi wenye watoto wanaosoma nchini China kutoruhusu watoto hao kurudi nchini humo kwasasa mpaka pale Serikali itakapotoa tamko baada ya kupata taarifa kutoka kwa Balozi wa Tanzania Nchini China Mbelwa Kairuki kuhusu hali inavyoendelea nchini humo kufuatia ugonjwa unao sababishwa na kirusi cha CORONA.
Waziri Mkuu amesema hayo Bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali liloulizwa na Mbunge wa Mafinga Mjini Cosato Chumi lilotaka kujua Serikali imejipangaje kukabiliana na kudhibiti ugonjwa huo kwa Tanzania kufutia muingiliano wa kibiashara baina ya Tanzania na China.
Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeimarisha mawasiliano kati ya Serikali na ubalozi wake nchini China na ubalozi wa China hapa nchini ili kupata taarifa za namna hali inavyoendelea nchini humo zitakazo saidia kutoa taarifa kwa wanafunzi hao kurejea nchini humo kuendelea na massomo yao hali ya ugonjwa huo itakapopungua.