Rais Dkt. John Magufuli ameipongeza Mahakama na wadau wake kwa hatua kubwa za kimaendeleo zilizopigwa katika kipindi cha miaka 4 iliyopita na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha Mahakama inaboreshwa zaidi.
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo tarehe 06 Februari, 2020 katika sherehe za kilele cha Wiki ya Elimu na Siku ya Sheria zilizofanyika katika ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Spika wa Bunge Mhe. Job Yustino Ndugai, Majaji Wakuu Wastaafu, Mabalozi wa nchi mbalimbali, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, viongozi wa taasisi mbalimbali, viongozi wa Dini na Viongozi wa Siasa.
Katika hotuba hiyo, Mhe. Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na mafanikio makubwa ya utekelezaji wa ahadi na maelekezo yake juu ya uboreshaji wa Mahakama yakiwemo kumaliza mrundikano wa mashauri mahakamani na kupunguza mrundikano wa mashauri yenye muda wa zaidi ya miaka 2 kutoka asilimia 12 hadi 5.
Mhe. Rais Magufuli amebainisha mafanikio mengine kuwa ni Serikali kuteua Majaji wapya 11 wa Mahakama ya Rufani, Majaji wapya 39 wa Mahakama Kuu na kuajiri Mahakimu wapya 396 ambao wamesaidia kupunguza tatizo la ucheleweshaji wa kesi, na pia amempongeza Waziri wa Katiba na Sheria kwa kuwapa Mahakimu 195 mamlaka ya kusikiliza mashauri ya Mahakama Kuu ambapo Mahakimu 98 walifanya kazi hiyo wamemaliza mashauri 1,132 kwa mwaka jana. Ameahidi kuwaangalia Mahakimu waliofanya kazi hiyo.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amepongeza hatua kubwa iliyopigwa na Mahakama katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambayo licha ya kupunguza tatizo la ucheleweshaji wa kesi na rushwa, pia imesaidia kuongeza maduhuri ya Serikali kutoka shilingi Bilioni 1.6 hadi kufikia shilingi Bilioni 2.5.
Maeneo mengine ni kuanzishwa kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ambapo katika maeneo inayofanya kazi idadi ya mashauri imepungua (mfano Mahakama ya Kisutu ambayo mashauri yanayofikishwa mahakamani yamepungua kutoka zaidi ya 1,500 kwa mwaka hadi kufikia 300), kutoa msamaha kwa wafungwa 38,801 hali iliyosaidia kupunguza msongamano magerezani na kuanzishwa kwa Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Ufisadi (Mahakama ya Mafisadi) ambapo tangu ianzishwe mwaka 2016 mashauri 119 yamesajiliwa, 89 yamemalizika, faini iliyolipwa ni shilingi Bilioni 13.6 na fidia shilingi Bilioni 30.6.
Kuhusu miundombinu, Mhe. Rais Magufuli amesema kwa miaka 4 Serikali imejenga Mahakama Kuu 2 (Mara na Kigoma), imekarabati Mahakamu Kuu 4 (Dar es Salaam, Shinyanga, Mbeya na Sumbawanga), imejenga Mahakama za Wilaya 15 na Mahakama za Mwanzo 11.
Mhe. Rais Magufuli amekiri kuwa pamoja na mafanikio hayo makubwa bado kuna changamoto na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuzishughulikia kadiri uwezo wa kifedha unavyo ruhusu.
Ametoa wito kwa Mahakama na wadau wengine yakiwemo Mabaraza ya Ardhi kutoa kipaumbele katika kushughulikia migogoro ya ardhi na dhuluma dhidi ya wanawake hasa wajane ambayo imekithiri hapa nchini. Amewataka Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya ambao ni wenyeviti wa kamati za mahakama katika maeneo yao kushirikiana vizuri na Mahakama katika kushughulikia kero mbalimbali za wananchi.
Kuhusu kaulimbinu ya mwaka huu isemayo “Uwekezaji na Biashara; Wajibu wa Mahakama na wadau katika kukuza uwekezaji na biashara” Mhe. Rais Magufuli ameipongeza Mahakama kwa kutambua safari ya Tanzania kujenga uchumi wa viwanda inapoelekea katika uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa ushirikiano mkubwa ambao Serikali inautoa kwa Mahakama na ameahidi kuwa Mahakama itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi ili kuhakikisha Watanzania wanapata haki yao ipasavyo.
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS) Dkt. Rugemeleza Nshala amesema TLS iliyotimiza miaka 65 tangu kuanzishwa kwake ina Mawakili 8,667 ambapo takribani asilimia 75 ni vijana. Hivyo kuna hitaji kubwa la kuwajengea uwezo wa kimaadili na uzoefu wa kazi za uwakili na hivyo TLS inahitaji kupata majengo na fedha za kujiendesha, mambo ambayo Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali itayaangalia.