- Wananchi wa kijiji cha Kalenge wilayani Uvinza wameishukuru kwa Serikali kukamilika ujenzi wa zahanati na hivyo kuwahepusha na vifo vitokanavyo na uzazi.
- Hayo yamebainishwa na wakazi wa eneo hilo wakati walipotembelewa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto-Idara Kuu Afya Dkt. Zainab Chaula ambaye ameanza ziara ya usimamizi shirikishi mkoani kigoma ambayo inafanywa na wizara ya afya pamoja na TAMISEMI.
- Akiongea kwa furaha bi. Marystela Chishako alisema kuwa wanaishukuru serikali kwani kwa kupata zahanati hiyo imewasaidia kupata huduma za afya ikiwemo huduma ya kujifungua ambayo awali walikua wakiifuata kigoma mjini.
- “Tunashukuru kwa serikali hii kutukumbuka mkoa wa kigoma,siku za nyuma mama akitaka kujifungua ilibidi aende kigoma mjini,ila hivi sasa tunajifungulia hapa hapa kwenye zahanati na tunapata huduma muhimu hapa hapa”.
- Aidha, alisema zahanati hiyo imewasaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto kwani kipindi cha nyuma walikua wakipata matatizo njiani kwa sababu walikua wakisafiri umbali mrefu na kupelekea kupata matatizo wakiwa njiani.
- Katika Ziara hiyo Katibu Mkuu Dkt.Chaula aliwahidi kulifanyia kazi ombi lao la kupatiwa kituo cha afya kwani wameshaomba kwa kufuata utaratibu kupitia mkoa.
- “Ninawapongeza kwa sababu mmejua umuhimu wa kuwa na kituo cha afya,kwahiyo maombi yataletwa wizara ya afya kutoka TAMISEMI,na katika ziara yangu nimeongozana nao hapa na nimepokea ombi hili najua ukitoa ahadi lazima utimize”.Alisema Dkt. Chaula
- Hata hivyo Katibu Mkuu huyo amesema atahakikisha wanapata fedha ili kutimiza ndoto za wananchi hao”mmefanya wajibu wenu na uzalendo mkubwa wa kuipenda nchi yenu kwa kujituma mpaka mmetenga eneo na kuweka mawe na mchanga, hivyo serikali itaongezea nguvu pale mlipoanzisha.
- Wakazi hao wametenga eneo la hekari ishiriki, kukusanya mawe pamoja na mchanga kwa kujitolea ili kuweza kujenga kituo cha afya ikiwa ni juhudi za kuiunga mkono serikali kwa kutatua changamoto za huduma za afya karibu na wananchi. Na.Catherine Sungura-Uvinza
Ad