Na. Majid Abdulkarim , Kiteto
Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Selemani Jafo amewataka wataalam wa afya kujipanga vema katika kutoa huduma nzuri kwa wananchi ili kutimiza adhima ya Mhe.Rais ya kuwatumikia watanzania.
Kauli hiyo ameitoa leo wakati wa ufunguzi wa kituo cha afya cha Sunya kilichopo wilayani Kiteto Mkoani Manyara.
Aidha Mhe. Jafo amewataka wananchi kuhakikisha wanalinda miundombinu ya kituo hicho ili dhamira ya Serikali ya kusogeza huduma za afya karibu na wananchi iweze kutimizwa .
Katika ufunguzinhuo Mhe.Jafo amesema kituo hicho kitakuwa msaada mkubwa sana kwa wananchi wa Sunya na Kiteto kwa ujumla sababu Wilaya hiyo ni imetawanyika na vituo viko mbali mbali na Kata ya Sunya ni miongoni mwa Kata za pembezoni Kutoka Makao Makuu ya Wilaya. “Kukosekana kwa kituo cha afya katika kata ya Sunya kulipelekea wakazi hao kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za Afya na wakati mwingine ilibidi wananchi hao kwenda Wilayani Kilindi Mkoani Tanga au kusafiri kilomita 125 kufuata huduma katika hospitali ya Wilaya
Aliongeza kuwa kituo hicho ni miongoni mwa vituo vilivyopewa kiasi cha shilingi milioni 400 na ujenzi umekamilika kwa kiwango kinachotakiwa” ameeleza Mhe. Jafo.
Aidha Mhe Jafo aliwataka wananchi kushirikiana katika kutunza miundombinu ya kituo hicho ili kusitokee uharibifu wowote na kila mtu kuwa mlinzi wa mwenzake ili kituo kiweze kuwa na manufaa kwa kizazi hiki na vizazi vijavyo,”alisisitiza Mhe. Jafo.
Katika hatua nyingine Mhe. Jafo amekagua ujenzi wa jengo la halmashauri na kumtaka mkandarasi Pacha Construction LTD kukamilisha ujenzi kwa wakati uliyopangwa. “Mkurugenzi ninachosisitiza hapa kazi ikamilike kwa wakati na niwaambie hili jengo likikamilika litakuwa ni miongoni mwa halmashauri zenye ofisi bora Tanzania,
Pia alimtaka Mkandarasi kupunguza gharama za ujenzi wa Jengo hilo ili liendane na hali ya sasa ameelekeza Mhe. Jafo.
Naye Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe.Tumaini Magese ameiomba Serikali kuwaongezea vituo vya afya viwili ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya kutokana na ukubwa wa Wilaya hiyo.