Rais Dkt. John Magufuli amesema kuwa mpaka kufikia leo tarehe 17 Mei, 2020 idadi ya wagonjwa wa corona nchini imepungua katika vituo mbalimbali akitaja takwimu hizo amesema kuwa katika Hospitali ya Amana (Dar es Salaam) iliyokuwa na wagonjwa 198 imebakiwa na mgonjwa 12, Hospitali ya Mloganzila iliyokuwa na wagonjwa 30 imebakiwa na wagonjwa 6.
Rais ameeleza kuwa katika Kituo cha Lulanzi (Kibaha) kulikuwa na wagonjwa zaidi ya 50 wamebaki 22, Agha Khan wamebaki wagonjwa 31, Hindu Mandal 16, Regency wamebaki 17, TMJ 7, Rabinisia 14, Moshono (Arusha) 11, Longido 0, Karatu 0, Buswelu 2, Misungwi 2, Ukerewe 0, Magu 0, Mkuyuni 0, Nyahunge 0, Sengerema 0, Kwimba 0, Bugando na Sekou Toure 2, Dodoma 2 (kutoka zaidi ya 40), Kongwa 0, Kondoa 0 nakadhalika. Na kwamba wagonjwa wengi wana hali nzuri.
Rais Dkt. John Magufuli amesema hayo wakati akizungumza na Waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Chato Mkoani Geita aliposali Ibada ya Jumapili iliyoongozwa na Mchungaji Thomas Paschal Kangeizi.
Rais Magufuli amesema endapo hali ya ugonjwa wa Corona itaendelea hivi Serikali inafikiria kufungua vyuo ili wanafunzi warudi vyuoni kuendelea na masomo na pia michezo itaruhusiwa kuendelea kufanyika hapa nchini
Aidha Rais amesema kuwa “Mimi namwamini Mungu na Mungu amejibu maombi yetu, tumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutusikiliza na tuendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huu wa Corona”
Amebainisha kuwa kuna idadi kubwa ya watalii wanaotaka kuja hapa nchini na ambao tayari wameonyesha nia ya kukata tiketi za kuja, hivyo ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na mamlaka zingine zinazohusika kutowazuia watalii na ndege zinazotaka kuleta wageni hapa nchini.
Amesisitiza kuwa viongozi na Watanzania wote wasiwe na hofu kubwa dhidi ya ugonjwa wa Corona kiasi cha kusababisha matatizo mengine ikiwemo kutowahudumia ipasavyo wagonjwa mbalimbali ambao baadhi wanaambiwa wana Corona ilihali hawajaambukizwa ugonjwa huo, ama kuwazuia watoa huduma wakiwemo Madaktari na Wauguzi wanaoshukiwa kuwa wameambukizwa Corona.
Amesema “wapo watu ambao wanaambiwa wana Corona lakini wakipimwa tena wanakutwa hawana” na amewataka viongozi waache kuwazuia watu kuzika kwa heshima marehemu wao kama ambavyo wanawazika watu waliokufa kwa magonjwa mengine yakiwemo ukimwi, kifua kikuu na surua.
“Hata mimi mtoto wangu alipata Corona lakini amepona, alikuwa anakula limau, tangawizi, anajifukiza mpaka amepona, kwa hiyo ugonjwa huu utasambaa na utakwisha, hatuwezi kufunga mipaka, sisi Tanzania tukifunga mipaka nchi zinazotuzunguka watapata shida, hata sasa tulipata tatizo la upungufu wa sukari, nimezungumza na Rais wa Uganda Mhe. Museveni na zimekuja tani 26,000 kwa meli hadi Mwanza, na tani nyingine 10,000 zimekuja kupitia bandari ya Dar es Salaam, tungefunga mipaka ingekuwaje?” amesema Mhe. Rais Magufuli
Amesisitiza kuwa Watanzania waendelee kuchapa kazi hasa kuzalisha chakula kwa wingi kwa kuwa majirani ambao wamefunga mipaka na wamewafungia watu wao (lockdown), pindi watakapofungua watahitaji chakula na watakuja Tanzania.
“Tutumie mvua hizi za mwisho zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwetu, kuzalisha mazao yanayokomaa haraka ili baadaye wenzetu watakapofunguliwa tuwauzie chakula, endeleeni kuchapa kazi” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Kuhusu uchunguzi uliofanyika katika Maabara ya Taifa, Mhe. Rais Magufuli amesema tume iliyoundwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu imefanya kazi nzuri na matokeo ya uchunguzi wake yatatangazwa na Waziri mwenyewe.
Mchungaji wa KKKT Usharika wa Chato Thomas Paschal Kangeizi amemshukuru Mhe. Rais Magufulu kwa kuungana nao katika Ibada, kuruhusu Makanisa kufanya Ibada na amemuahidi kuwa Wataendelea kumuombea ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ulinzi wa Mwenyezi Mungu.
Katika Ibada hiyo Mhe. Rais Magufuli na Mkewe Mama Janeth Magufuli wamechangia shilingi Milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa jipya la KKKT Chato na amechangia shilingi Milioni 1 kwa ajili ya kwaya 3 zilizoimba katika Ibada hiyo.