Kampuni ya Barrick imeilipa Tanzania dola milioni 100, sawa na takriban sh. bilioni 250, ikiwa ni sehemu ya malipo ya dola milioni 300 ambazo Kampuni hiyo ya Madini ilikubali kulipa kama fidia ya kodi.
Mfano wa Hundi ya kiasi hicho cha fedha imekabidhiwa na Meneja Mkazi wa Kampuni ya Barrick, Bw. Hilaire Diarra kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, kwa niaba ya Serikali, Jijini Dodoma tarehe 27 Mei, 2020.
Akizungumza baada ya kupokea hundi hiyo mbele ya viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Mwenyekiti wa Timu ya Serikali ya Majadiliano na Barrick ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi na Kamati yake, Dkt. Mpango alisema tukio hilo ni mwanzo wa makubaliano ya mkataba wa msingi kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni hiyo yaliyofikiwa Disemba 19, 2019 na kusainiwa rasmi Januari 24, 2020.
Dkt. Mpango aliyataja makubaliano mengine yaliyofikiwa kati ya Serikali na kampuni hiyo kuwa ni kuundwa kwa Shirika la Madini la Twiga lenye umiliki wa pamoja likalofanya kazi nchini katika kusimamia uendeshaji wa migodi ya Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara pamoja na migodi mingine nchini ambapo Serikali ya Tanzania itashiriki katika utoaji wa maamuzi kuhusu uendeshaji wa migodi, mipango, manunuzi pamoja na masoko ya madini.
“Tulikubaliana kuhakikisha kuwa faida za kiuchumi zinazotokana na migodi ya Bulyanhulu, Buzwagi pamoja na North Mara zigawanywe kwa msingi wa usawa wa asilimia 50 kwa 50 kati ya washirikania ambapo hisa za Serikali zinazotokana na faida za kiuchumi zitatolewa katika mfumo wa mrabaha, kodi pamoja na kupata asilimia 16 ya faida kutokana na makampuni hayo kufanya kazi nchini” alisema Dkt. Mpango
Dkt. Mpango alisema mbali na makubaliano hayo, kampuni ya Barrick imekubali kutoa kiasi cha dola za Marekani milioni 5 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa Mtambo wa kuchakata madini nchini (smelter).
“Kampuni ya Barrick pia imekubali kuanzisha ushirikiano na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuahidi kutoa hadi dola milioni 10 kwa kipindi cha miaka kumi kwa ajili ya utoaji wa mafunzo yanayohusu sekta ya madini”, aliongeza Dkt. Mpango.
Alisema Kampuni ya Barrick ilikubali kutoa dola 6 kwa kila ounce ya madini itakayouzwa (ikijumuisha mchango kwenye Mfuko wa Mandeleo ulioanzishwa na Kampuni ya Barrick Tanzania) ili kusaidia jamii zinazozunguka maeneo ya migodi pamoja na kutoa kiasi cha dola milioni 40 kwa ajili ya kuboresha kipande cha barabara kati ya Bulyanhulu na Mwanza na kujenga nyumba na miundombinu yake.
“Naipongeza Kampuni ya Barrick kwa kuanza kutekeleza makubaliano haya na natoa wito kwa kampuni nyingine za madini na wawekezaji wengine katika sekta hiyo kuiga mfano mzuri uliooneshwa na Kampuni hii katika kuhakikisha kunakuwa na hali ya usawa katika uendeshaji wa shughuli za madini nchini kwa faida ya pande zote mbili” alisisitiza Dkt. Mpango.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Doto James alisema kuwa fedha hizo tayari zimeshapokelewa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.
Kwa upande wake Rais na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Barrick, Dkt. Dennis Mark Bristow ambaye alikuwa akifuatilia makabidhiano hayo kwa njia ya mtandao na kutoa hotuba yake akiwa nchini Afrika Kusini alimpongeza Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Timu yake kwa kufanikisha majadiliano yaliyosaidia kuanzishwa kwa ushirikiano wa dhati kati ya Kampuni yake na Serikali.
Alisema kuwa wataendeleza ushirikiano wao na Tanzania na kwamba wanaamini kuwa ushirikano huo utakuwa wa mfano si tu kwa Afrika bali utakuwa ni ushirikiano wa mfano kwa Dunia nzima.
Aliahidi kuendelea kuboresha miundombinu ya maeneo ya migodi wanayomiliki nchini na kueleza kuwa wanajiolojia wanafanyakazi kwa bidii ili kuirudisha hadhi ya Tanzania kuwa kituo kikubwa cha uzalishaji dhahabu duniani.