Serikali imesema Ushuru wowote unaotolewa kwenye Maeneo ya Migodi Nchini ni lazima uthibitishwe na Maafisa Madini walioko kwenye maeneo husika.
Tamko hilo lilitolewa Mei 24, 2020 na Waziri wa Madini Doto Biteko wakati akizungumza na Wachimbaji Wadogo wa Madini ya Dhahabu eneo la Lusu Wilayani Nzega Mkoa wa Tabora alipotembelea eneo hilo kuangalia shughuli za uchimbaji madini.
Aidha, tamko hilo linafuatia kuwepo kwa malalamiko toka kwa wachimbaji wanaofanyakazi kwenye Leseni za baadhi ya Wachimbaji ambao walimlalamikia Waziri Biteko kutozwa kodi na wenye leseni hizo na hivyo kuomba ufafanuzi juu ya suala hilo.
Waziri Biteko alisisitiza kwa kuwataka Maafisa hao kuhakikisha Ushuru unaotolewa ni ule tu uliopo Kisheria na kuhakikisha wanasimamia jambo hilo.
Na Asteria Muhozya, Nzega
Akifafanua kuhusu suala la mrabaha wa mawe unaotozwa na Serikali alieleza kuwa, wachimbaji wasio rasmi wanalazimika kulipia mrabaha wa mawe isipokuwa wenye Leseni wanatakiwa kulipia mrabaha wa dhahabu baada ya kukamilisha hatua zote.
” Wale msio rasmi mjue mkigawana mawe na Serikali itakuwepo mnagawana nayo isipokuwa mwenye Leseni yeye tutamwomba mrabaha wetu mwishoni. Ukitaka kulipa mrabaha mara moja chimba kwenye Leseni, mkichimba bila utaratibu tutagawana kwenye mawe na kwingine,” alisisitiza Waziri Biteko.
Pia, aliendelea kuwasisitiza wachimbaji nchini kuyatumia Masoko ya Madini yaliyoanzishwa katika maeneo mbalimbali kufanya biashara ya madini.
Akijibu ombi la wachimbaji hao kupelekewa Wataalam wa masuala ya Utafiti ili kuwawezesha kujua mwelekeo wa miamba na hivyo kuchimba kwa tija, alisema Wizara itaangalia namna ya kufikisha Mtambo wa Kuchoronga katika eneo hilo baada ya Shirika la Madini la Taifa ( STAMICO) kukamilisha kazi za kandarasi za uchorongaji zinazoendelea katika maeneo mengine.
Katika hatua nyingine, alipongeza wachimbaji kwa kulipa mrabaha wa Serikali na hivyo kuwezesha makusanyo ya shilingi Bilioni 2.7 hadi kufikia Aprili 30, sawa na asilimia 122 na hivyo kuvuka lengo la makusanyo ya shilingi bilioni 2.2 zilizopangwa kukusanywa Mwaka wa fedha 2019/2020.