Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu ametoa agizo kwa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kuongeza idadi ya mabango ya barabarani yanayoonyesha tahadhari na faini kwa madereva watakaogonga wanyamapori katika barabara ya Babati kuelekea Arusha.
Ametoa agizo hilo katika wilaya ya Babati mkoani Manyara katika mkutano wa Wadau wa Uhifadhi uliowakutanisha Wataalamu mbalimbali kujadili namna ya kulinda mapito asili ya wanyamapori (shoroba) pamoja na maeneo mengine muhimu ya wanyamapori ambayo yapo hatarini kutoweka kufuatia kushamiri kwa shughuli za kibinadamu Kanyasu amesema kukosekana kwa tahadhari hizo kunatishia kuharibika kwa ikolojia ya Tarangire na Manyara kutokana na idadi kubwa ya wanyamapori kuuawa kwa kugongwa na magari kila siku.
Kwa mujibu wa takwimu jumla ya wanyamapori 588 wakiwemo simba na twiga waliuawa mwaka jana kwa kugongwa na magari yanayopita kwa spidi katika barabara hiyo
Kufuatia hali hiyo, Mhe.Kanyasu ameitaka TANAPA kwa kushirikiana na Jumuiya ya Wanyamapori ya Burunge kukutana na Uongozi wa TANROAD ili waweze kutekeleza agizo hilo la uongezaji mabango katika barabara hiyo.
Akizungumzia mazimio ya Mkutano huo, Mhe. Kanyasu amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii kuunda kikosi kazi cha wataalamu mbalimbali kwa ushirikiano wa ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Babati kutambua mipaka ya shoroba katika vijiji
Mbali na maazimio hayo, Mhe, Kanyasu amemtaka Mkuu wa wilaya ya Babati Kuhakikisha maeneo ambayo tayari yanatambulika kuwa ni shoroba yalindwe ili yasiendelee kuvamiwa.
Aidha, Mhe.Kanyasu amemtaka Mkuu wa wilaya ya Babati kuhakikisha anatoa maagizo kwa Uongozi wa vijiji vinavyozunguka shoroba hawagawi maeneo ambayo ni shoroba kwa Wananchi kwa ajili ya shughuli za kibinadamu ikiwemo ujenzi na kilimo.