UFARANSA YAIPATIA SERIKALI MKOPO NAFUU WA EURO MILIONI 70 KUJENGA MRADI WA MAJI MJINI MOROGORO

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James (kushoto) na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) Bi. Stephanie Mouen Essombe, wakibadilishana hati za Mkataba wa mkopo wenye masharti nafuu wa  Euro milioni 70 (Sh. za Tanzania bilioni 175.6) kwa ajili ya kugharamia mradi wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira mjini Morogoro (MORUWASA), jijini Dodoma.

Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) zimetiliana saini mkataba wa mkopo wenye masharti nafuu wa Euro milioni 70, sawa na takriban shilingi za Tanzania bilioni 175.6 kwa ajili ya kugharamia Mradi wa Maji Safi na Usafi wa Mazigira Mjini Morogoro (MORUWASA).

Mkataba wa mkopo huo umesainiwa Jijini Dodoma na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James kwa upande wa Serikali na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa, Bi. Stephanie Mouen Essombe.

Ad

Bw. James alisema mkopo huo utawezesha wakazi wa Mjini Morogoro wapatao 722,010 kupata maji safi na salama kupitia upanuzi wa mfumo wa usambazaji wa Maji kutoka Bwawa la Mindu.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James (kushoto) na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa Bi. Stephanie Mouen Essombe, wakisaini mkataba wa mkopo wenye masharti nafuu wa  Euro milioni 70 (Sh. za Tanzania bilioni 175.6) kwa ajili ya kugharamia mradi wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira mjini Morogoro (MORUWASA), jijini Dodoma. Anaye waongoza ni Mwanasheria wa Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Nyanzala Nkinga 

Alisema kukamilika kwa mradi huo kutawezesha upatikanaji wa Maji kutoka mita za ujazo 33,000 hadi kufikia mita za ujazo 108,000 kwa siku pamoja na kuwezesha Mji wa Morogoro kupata kiwango cha mahitaji ya maji safi kinachokadiriwa kuwa mita za ujazo 126,253 kwa siku, ifikapo mwaka 2035.

“Mradi pia utaongeza upatikanaji wa huduma za majitaka kutoka kiwango cha sasa cha asilimia 5 hadi asilimia 15 kwa wakazi wa mjini Morogoro”, alifafanua.

Bw. James alisema Tanzania imekuwa ikinufaika na ufadhili wa AFD hususan katika sekta za Nishati, Maji, Usafirishaji na Kilimo kupitia idadi ya miradi  mbalimbali inayoendelea na ile inayotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James (katikati) akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Maji Prof. Kitila Mkumbo (kushoto) na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) ) Bi. Stephanie Mouen Essombe wakati wa hafla ya kusainiwa kwa mkataba wenye masharti nafuu ambapo AFD imeikopesha Tanzania Euro milioni 70 sawa na shilingi za Tanzania bilioni 175.6 kwa ajili ya Mradi wa Maji safi na Usafi wa Mazingira Mjini Morogoro (MORUWASA).

Na Farida Ramadhani-WFM, Dodoma

Alisema miradi 7 inayoendelea kutekelezwa katika sekta mbalimbali hapa nchini kupitia misaada na mikopo inayotolewa wa Shirika hilo inafikia takriban Euro milioni 154.5 sawa na shilingi bilioni 387.6.

“Miradi 6 yenye thamani ya Euro milioni 141.4 kupitia ufadhili wa AFD imekamilika na kuna miradi mingine 12 yenye thamani ya Euro milioni 1,021.7 ambayo tuko kwenye mazungumzo na AFD katika sekta ya Nishati, Maji, Kilimo Usafiri wa mwendokasi Jijini Dar es Salaam, miundombinu ya viwanja vya ndege na Usafi wa mazingira Jijini Dare salaam” alisema Bw. James.

Aliishukuru Serikali ya Ufaransa kupitia Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) kwa ufadhili huo muhimu, ambao utachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya nchi na kupunguza umaskini na kuahidi kuwa Serikali itafuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha kwamba fedha zitakazotolewa zinatumika kama ilivyokusudiwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Bi. Stephanie Mouen Essombe aliahidi kuwa shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania ili kuhakikisha inafikia malengo yake katika kuboresha maisha ya wananchi hasa katika upatikanaji wa maji.

“Ushirikiano wa Tanzania na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) ulioanza miaka 20 iliyopita umezidi kuimarika ambapo katika kipindi cha miaka 10 iliyopita Shirika limewekeza kiasi cha Euro milioni 258 sawa na takriban Sh. bilioni za Tanzania 655” alisema Bi. Essombe.

Alisema mradi huo umelenga kupanua Bwawa la Mindu linalochangia upatikanaji wa maji yanayotumika katika Mji wa Morogoro kwa asilimia 70 pamoja na kuboresha mfumo wa huduma ya maji taka katika mji huo.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Prof. Kitila Mkumbo alisema kuwa mkopo huo utatatua changamoto ya maji ambayo ilikuwa kilio cha muda mrefu kwa wananchi wa Morogoro.

Alisema mkopo huu unafaida nyingi nchini ikiwemo kutoa ajira pamoja na kutoa fursa kwa viwanda vya ndani kwa sababu vifaa vitakavyotumika kutekeleza mradi huo wa kihistoria vitanunuliwa ndani ya nchi.

Alisema hivi sasa Serikali inatekeleza miradi ya maji 1,423, miradi 792 imekamilika na miradi 631 inaendelea na kwamba mradi huo wa maji wa Mji wa Morogoro utakuwa mkombozi mkubwa wa wananchi wa mji huo.

Alisema upatikanaji wa fedha hizo ambazo mjadala wa kupata mkopo umechukua zaidi ya miaka minne utawezesha kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maji nchini ambapo hivi sasa kiwango cha upatikanaji wa maji vijijini kimefikia asilimia 85 ya lengo la asilimia 95 iliyoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM huku katika miji kiwango kimefikia asilimia 70.1 kati ya lengo la asilimia 85 ifikapo mwishoni mwa mwaka 2020

Ad

Unaweza kuangalia pia

RAIS MAGUFULI AKABIDHI NDEGE AINA YA TAUSI KWA MARAIS WASTAAFU KATIKA IKULU YA CHAMWINO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akimkabidhi Hati ya …

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.