WAZIRI KAIRUKI -CHANGAMKIENI FURSA ZA UWEKEZAJI WA KUZALISHA MAFUTA YA ALIZETI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri (Uwekezaji), Angellah Kairuki akipataa maelezo kuhusu kifaa cha kupima kiwango cha vitamin ‘A’ katika alizeti kutoka kwa Afisa Viwango, Upendo Mganda wakati wa ziara yake ya kikazi alipotembelea na kukagua kiwanda kinachozalisha mafuta ya kula ya alizeti cha SUNSHINE chenye kuzalisha mafuta aina ya Sunbelt.

Na Mwandishi wetu

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Uwekezaji nchini, Angellah Kairuki ametoa rai kwa Watanzania kuwekeza katika sekta ya mafuta ya kula kwa kuzingatia uhitaji na soko lililopo ndani na nje ya nchi.
Ametoa rai hiyo Mei 28, 2020 alipotembelea na kukagua kiwanda cha kuzalisha mafuta ya kula cha SUNSHINE kinachozalisha mafuta yanayotengenezwa kwa kutumia malighafi ya alizeti yanayoitwa Sunbelt kilichopo katika eneo la Zuzu Jijini Dodoma.
Akiwa katika ziara hiyo, yenye lengo la kukagua, kusikiliza na kutatua changamoto za wawekezaji nchini.Waziri Kairuki alipongeza uwekezaji katika kiwanda hicho chenye uwezo wa kuzalisha tani 25 kwa siku na kilichowekeza zaidi ya shilingiBilioni 230.
“Niwapongeze kwa uwekezaji mkubwa mlioufanya katika eneo hili tangu mwaka 2015 na hii inaleta chachu kwa wawekezaji wazawa kuona fursa na soko la malighafi wanazozalisha hasa zao la alizeti,”alisema Waziri Kairuki
Aliongezea kuwa, ni vyema watanzania wakaendelea kuchangamkia fursa ya kilimo cha zao la alizeti kwa kuzingatia uhitaji mkubwa wa mafuta ya kula nchini kwani nchi imekuwa ikipoteza zaidi ya shilingi bilioni 443 kwa mwaka kwa kuagiza mafuta nje ya nchi.
Aidha Waziri alibainisha kuwa uwekezaji huo ni miongoni mwa fursa muhimu na kuwataka wenye uwezo kulima zao hilo kwa wingi kuchangamkia fursa hiyo kwa vile zao hilo linastawi katika ukanda huo.
Alitumia fursa hiyo kuendelea kuwasihi wataalam wa masuala ya kilimo kutoa elimu kwa umma kuhusu kilimo bora cha zao hilo ili kuwa na utaalam wa kutosha kuhusu kilimo cha zao hilo ili kutumia mbinu za kisasa na zenye kuzingatia viwango vinavyotakiwa.
Akitoa taarifa ya kiwanda hicho, Meneja Biashara na Maendeleo wa kiwanda hicho Bw. Krishna Urs alieleza changamoto wanayokabiliana nayo ni uhaba wa malighafi kwa ajili ya uzalishaji na kuendelea kutoa wito kwa wadau kuitumia fursa ya kilimo cha zao hilo ili kuendana na mahitaji halisi.

Ad
Ad

Unaweza kuangalia pia

BANDARI YA DAR ES SALAAM INAPANUKA NA KUIMARIKA: HATUA MUHIMU KWA UCHUMI WA TANZANIA

Bandari ya Dar es Salaam ni kitovu muhimu cha biashara na uchumi wa Tanzania, na …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *