DKT. CHAULA AAHIDI KULETA MABADILIKO SEKTA YA MAWASILIANO

Baadhi ya wafanyakazi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano) wakiimba kwa furaha kumpongeza na kumkaribisha Katibu Mkuu wao, Dkt. Zainabu Chaula (hayupo pichani) kwa kuteuliwa kuongoza Sekta hiyo wakati wa kikao cha wafanyakazi kilichofanyika kwenye ukumbi wa TBA, Dodoma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano) Dkt. Zainabu Chaula ameahidi kuleta mabadiliko chanya katika Sekta ya Mawasiliano  na kuwataka watumishi wa Sekta hiyo kuuvua unyonge na kufanya kazi kwa kufuata miongozo na kushirikiana katika kutekeleza wajibu na majukumu yao kwa bidii, weledi na uzalendo. 

Dkt. Chaula ameyasema hayo mwishoni mwa wiki katika kikao chake na watumishi wa Sekta hiyo alichokifanya kwa mara ya kwanza tangu alipoteuliwa kuongoza Sekta hiyo tarehe 22 mwezi Aprili mwaka huu ambapo  kikao hicho kimefanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Wakala wa Majengo (TBA), Dodoma

Ad

Katika kikao hicho, Dkt. Chaula ametoa rai kwa watumishi wa Sekta ya Mawasiliano kuboresha mahusiano yao mahali pa kazi ikiwa ni pamoja na kupeana taarifa sahihi na kwa wakati ili watumishi wote wawe na uelewa wa pamoja kuhusu majukumu na miradi inayotekelezwa na Sekta hiyo.

Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Mawasiliano, Bi Laurencia Masigo, akiwasilisha hoja za wafanyakazi kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Zainabu Chaula (hayupo pichani) wakati wa kikao cha wafanyakazi kilichofanyika kwenye ukumbi wa TBA, Dodoma

Pia, amesisitiza kuboresha mahusiano mazuri kati ya Sekta na taasisi zake ambazo ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Shirika la Posta Tanzania (TPC), Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na Tume ya TEHAMA (ICT Commisison) ili kuwa na ushirikiano na kujenga uelewa wa pamoja katika kutekeleza majukumu ya Serikali ya kuhudumia wananchi.

“Mahusiano yetu tunayajenga sisi wenyewe, iwe ni mahusiano ya ndani ya Sekta au kati ya Sekta na taasisi inazozisimamia, ninataka kila mtu awajibike katika nafasi yake ili mwishoni aweze kusema ameifanyia nini Sekta ya Mawasiliano kwa kuwa mahusiano mazuri mahali pa kazi ni tunu ya utendaji mzuri wa majukumu kazini,” amesisitiza Dkt. Chaula

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Jim Yonazi amesisitiza watumishi kupendana na kushirikiana ili kufanya kazi katika mazingira rafiki na yenye utashi zaidi.

Ameongeza kuwa milango ya ofisi yake na ya Dkt. Chaula ipo wazi kusikiliza na kushughulikia kero na matatizo ya watumishi na kuwaasa watumishi wasikae na kero zao moyoni.

Naye mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Mawasiliano, Bi. Laurencia Masigo amempongeza Dkt. Chaula kwa kurejesha imani na matumaini kwa wafanyakazi wa Sekta hiyo kwa kipindi kifupi tangu ameteuliwa kuongoza Sekta hiyo na kuahidi kuwa wafanyakazi hawatamuangusha na wako tayari kufanya kazi kwa bidii na kujituma ili kuhakikisha kuwa Sekta ya Mawasiliano inaendelea kukua, kuchangia pato la taifa na kuhudumia wananchi.

Ad

Unaweza kuangalia pia

Mradi wa Magari ya Mwendo Kasi, Kuboresha Usafiri, Uchumi, na Mazingira Tanzania

Mradi wa magari ya mwendo kasi nchini Tanzania umekuwa na faida nyingi za kijamii, kiuchumi, …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *