Mkurugenzi Mtendaji TANESCO Dkt. Tito Mwinuka akiwa katika ziara ya ufuatiliaji na ukaguzi wa Mradi wa kusafirisha umeme kutoka Bulyanhulu hadi Geita kilovolti 220 amesema TANESCO inatarajia kukusanya takriban Shilingi bilioni 6 za ziada katika mauzo ya umeme Mkoani Geita.
Dkt. Mwinuka alisema kiasi hicho cha fedha ni kutoka katika Mgodi wa Geita Gold Mining (GGM) baada ya Mgodi huo kuunganishwa na kuongeza GGM bado unatumia umeme ghali wa mafuta mazito ukilinganisha na umeme wa TANESCO utakaopatikana baada ya kukamilika.
”Kupitia mradi huu tunatarajia kukusanya takriban bilioni 6 na zaidi kwa mwezi kutoka kwa GGM pekee ukiachana na Migodi mingine na wateja wengine wa Mkoa wa Geita”, alisema Dkt. Mwinuka.
Aliongeza lengo la ziara hiyo ni kukagua na kuhamasisha kasi ya utekelezaji wa mradi wa Bulyanhulu- Geita ambao ni muhimu kwa TANESCO na Taifa kwa ujumla.
Aidha, matumizi ya Mgodi wa GGM pekee ni Megawati 30 ambazo ni sawa na matumizi ya Mkoa mzima wa Morogoro.
Aliongeza kukamilika kwa mradi wa Bulyanhulu – Geita kutatuwezesha TANESCO kufikisha umeme mwingi Mkoani Geita na hivyo kuunganisha Wateja wakubwa wengi zaidi ikiwemo migodi mikubwa ya GGM na Stamigold- Biharamulo.
Dkt. Mwinuka aliongeza mradi huo unatarajiwa kukamilika katika kipindi kifupi kijacho.
Mradi wa Bulyanhulu – Geita unatarajiwa kufungua fursa za uwekezaji katika Mikoa ya ya Kaskazini Magharibi mwa nchi ambayo ni Geita, Kigoma na Kagera.
Aidha, miradi mingine ya vituo vya Kupokea na Kusafirisha Umeme huo kutoka Geita hadi Nyakanazi Kigoma na Nyakanazi kuelekea Rusumo Kagera tayari imeanza.