WATANZANIA WAMEANZA KUNUFAIKA NA MRADI WA JNHPP HATA KABLA HAUJAKAMILIKA – KATIBU MKUU NISHATI

Veronica Simba – Dodoma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Zena Said amesema kuwa mradi mkubwa wa kufua umeme wa maji wa Julius Nyerere (JNHPP) umeanza kuwanufaisha Watanzania hata kabla ya kukamilika.

Ad

Ameyasema hayo kwa njia ya simu, leo Juni 22, 2020 alipofanya mahojiano na mwandishi wa habari hii kuhusu ziara ya Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali waliyoifanya Juni 20, mwaka huu kukagua maendeleo ya Mradi huo ulioko Rufiji, mkoani Pwani.

Mhandisi Said ameyataja mafanikio hayo kuwa ni ajira kwa Watanzania pamoja na matumizi ya malighafi za ndani ya nchi, katika ujenzi wa Mradi husika.

Amesema kuwa Ujumbe wa Makatibu Wakuu hao walioshiriki ziara husika, ulifurahishwa kujionea kwamba asilimia kubwa ya wafanyakazi walioko katika Mradi huo ni Watanzania. Aidha, walifurahishwa kuona kuwa malighafi zinazotumika zinatoka Tanzania.

“Nchi yetu imeanza kunufaika kabla Mradi huu haujakamilika, hususan katika upande wa wafanyakazi na malighafi. Kwahiyo, uchumi umeanza kukua katika hatua hii ya utekelezaji wa Mradi,” amesema.

Ameongeza kuwa, Mradi utakapokamilika, Serikali inatarajia kupata umeme wa uhakika na wenye gharama nafuu ambao utasaidia zaidi katika kuendesha viwanda vilivyopo pamoja na kuhamasisha vingine vije kuwekeza.

Katibu Mkuu huyo mwenye dhamana na Mradi wa JNHPP, amemshukuru Rais John Magufuli kutenga fedha za ndani kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kimkakati, ukiwemo huo wa Julius Nyerere, akisema kuwa ni miradi ambayo itaipeleka nchi yetu mbele.

Akizungumzia manufaa zaidi yatakayopatikana baada ya ujenzi wa Bwawa katika Mradi husika kukamilika; amesema nchi itaingia kwenye ramani siyo tu ya Afrika bali pia ya dunia ikiwa ni miongoni mwa nchi zenye mabwawa makubwa ya kuzalisha umeme wa uhakika.

Awali, akizungumza baada ya ziara hiyo ya Makatibu Wakuu, Kiongozi wa Msafara, Prof. Sifuni Mchome, ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, alipongeza hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa Mradi husika, akisema wameridhishwa na kufurahishwa na maendeleo yake.

“Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu John Pombe Magufuli kwa maono haya makubwa ambayo tunaamini yatakapokamilika, Taifa litakuwa limefunguka na kazi mbalimbali zitakuwa zinaendelea kufanyika katika kujenga uchumi wetu, ili kufikia azma yetu ya uchumi wa kati ifikapo 2025.”

Prof. Mchome alitumia fursa hiyo kuwahakikishia Watanzania kuwa Mradi uko katika hatua nzuri na kwamba utatekelezwa kulingana na ratiba yake, hatimaye kupata umeme ambao Taifa linautegemea.

Ziara ya Makatibu Wakuu hao katika Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere, ni mwendelezo wa ziara za viongozi mbalimbali wa Serikali zinazolenga kuhakikisha Mradi huo unatekelezwa kikamilifu na kwa wakati, kama Serikali ilivyoahidi.

Ad

Unaweza kuangalia pia

BANDARI YA DAR ES SALAAM INAPANUKA NA KUIMARIKA: HATUA MUHIMU KWA UCHUMI WA TANZANIA

Bandari ya Dar es Salaam ni kitovu muhimu cha biashara na uchumi wa Tanzania, na …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *