Hafsa Omar-Morogoro
Naibu waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Julai 2,2020 amefanya ziara ya ukaguzi ya maendeleo ya ujenzi wa Mradi mkubwa wa kufua Umeme kwa Maji wa Julius Nyerere(JNHPP) unaotekelezwa kwenye mto Rufiji.
Katika ziara yake hiyo, aliambatana na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhandisi Stella Manyanya pamoja na viongozi mbalimbali wa Wizara ya Nishati.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza ukaguzi wa mradi huo alisema, ameridhishwa na hatua iliyofikiwa katika mradi huo hatua ambayo inaleta matumani ya kumalizika kwa wakati kwa mradi huo.
“Sisi Wizara ya Nishati tutaendelea kusimamia mradi huu kikamilifu tena kwa ari kubwa,ili tutimize lengo la Rais wetu kuwa mradi huu ukamilike kwa wakati na utakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa, kwahiyo niwapongeze sana wakandarasi kwa kufanya kazi nzuri mpaka sasa,”alisema Mgalu.
Alisema, mradi huo utakapomalizika unatarajiwa kuzalisha umeme wa megawati 2115, umeme huo ambao utakuwa mkombozi kwa wenye viwanda, wafanyabiashara pamoja na wananchi wa kawaida nchini kwasababu utakuwa umeme wa bei nafuu na utakaozalishwa kwa wingi.
Aidha, alisema moja ya faida kubwa ya mradi huo mpaka sasa ni kutoa ajira kwa watanzania ambapo zaidi ya watanzania 3000 wameajiriwa katika mradi huo ambao unatarajia kutoa ajira zaidi ya 6000.
Aliendelea kuelezea faida za mradi huo, ikiwa pamoja na kutoa fursa kwa makampuni ya wazawa ambayo yanauza bidhaa zao kwenye mradi huo, ambapo bidhaa nyingi zinazotumika katika mradi huo zinazalishwa nchini.
Pia, ameyataka makampuni aliyopewa kazi mbalimbali katika mradi huo kufanya kazi kwa bidii kwa kushirikiana na mkandarasi wa mradi huo ili kufanya kazi vizuri na mradi huo ukamilike kwa wakati kama ilivyopangwa.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhandisi Stella Manyanya, amesema Wizara yao ni mdau mkuu wa mradi huo kwasababu umeme utakaozalishwa kwenye mradi huo utawanufaisha sana wazalishaji viwandani pamoja na wafanyabiashara nchini.
Aidha, ametoa wito kwa Watanzania kuwekeza katika viwanda na kwenye biashara zitakazotumia nishati ya umeme kwani umeme wa uhakiki unatarajia kupatikana mara baada ya kumaliza mradi huo ambao utazalisha umeme mwingi.
Alieleza kuwa, mara baada ya kumaliza mradi huo utasaidia kupunguza gharama za uendeshaji wa viwanda nchini kwa kupata umeme wa uhakika wa gharama nafuu na kuweza kuendesha biashara zao kwa faida kubwa.
Aliongeza kuwa, amefurahishwa na mahusiano mazuri kati ya mkandarasi wa mradi huo pamoja na Watanzania wanaofanya kazi katika mradi, na kuwataka vijana ambao wanapata ujuzi kwenye mradi huo kutumia ujuzi watakaoupata kuzalisha miradi ya umeme midogo midogo.