HAKUNA KUHUISHA HATI ZA MIAKA 33 KWA WAMILIKI WA ARDHI WASIOENDELEZA VIWANJA- WAZIRI LUKUVI


Na Munir Shemweta, WANMM GEITA

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amewataka Makamishna Wasaidizi wa Ardhi katika ofisi za ardhi za mikoa nchini kuhakikisha wamiliki wote wa ardhi wasioendeleza viwanja vyao tangu kumilikishwa hawahuishi miliki zao za miaka 33 ili kupatiwa za miaka 99.

Lukuvi ametoa kauli hiyo jana mkoani Geita wakati akizindua ofisi ya ardhi mkoa wa Geita ikiwa ni mfululizo wa uzinduzi wa ofisi hizo nchini. Uzinduzi wa ofisi ya ardhi Geita umeenda sambamba na ule wa mkoani Kagera uliofanywa na Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula. 

Alisema, kuna wamiliki wa ardhi katika maeneo mbalimbali katika mikoa wameshindwa kuchukua hati za viwanja na wengi viwanja vyao ni vya miaka 33 na kutolea mfano wa mkoa wa Geita wenye zaidi ya wamiliki 30,000 huku baadhi yake wakishindwa maendelezo yoyote jambo alilolieleza limeikosesha  serikali mapato yatokanayo na kodi ya ardhi.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akikata utepe kuzindua ofisi ya ardhi mkoa wa Geita jana. Wa tatu kulia ni Mbunge wa jimbo la Bukombe mkoa wa Geita ambaye ni Waziri wa Madini Doto Biteko na wa pili kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Geita Josephat Maganga.

“Nawaagiza Makamishna Wasaidizi wa ardhi wa mikoa kuhakikisha  wamiliki woteb wa ardhi wasioendeleza maeneo yao wasihuishwe hati zao, kama kwa muda wa miaka 33 umeshindwa kuweka hata tofali huwezi kujenga tena, hatukutoa ardhi kwa mtu kama land bank” alisema Lukuvi.

Kwa mujibu wa Waziri Lukuvi,  wananchi walioendeleza viwanja vyao Makamishna wa mikoa  wanatakiwa kuhakikisha hati zao za miaka 33 zinahuishwa na kupatiwa zile za miaka 99 ili waweze kuzitumia kwa shughuli za kiuchumi kama kuchukua mikopo ya muda mrefu benki.

Sambamba na hatua hiyo, Waziri Lukuvi aliwataka Makamishna Wasaidizi wa ardhi katika ofisi za ardhi za mikoa kumpatia gharama halisi za upimaji kufuatia usambazaji vifaa vya upimaji uliofanywa na wizara yake kwenye ofisi hizo.

Ad
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akimkabidhi hati ya ardhi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Geita Mji Mhandisi Modest Apolinary wakati wa uzinduzi ofisi ya ardhi katika mkoa wa Geita jana. Lukuvi aliagiza wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kupima na kumilikishwa maeneo yao ili kuepuka migogoro ya ardhi. (PICHA ZOTE NA MUNIR SHEMWETA WIZARA YA ARDHI)

Alisema, kwa sasa gharama za upimaji katika halmashauri mbalimbali za wilaya hazina uhakika kutokana na kila eneo unapofanyika upimaji kuwa na kiwango chake alichokieleza kuwa kinawaumiza sana wananchi hasa wale wanyonge.

” haiwezekani serikali inunue vifaa vya zaidi ya bilioni 3 halafu mwananchi anaumizwa, yaani vifaa vya upimaji vinakodishwa na halmashauri kwa makampuni kwa gharama ya shilingi laki mbili na nusu   kwa siku na gharama hizo anazibeba mwananchi ni lazima gharama zishuke sasa” alisema Lukuvi

Aidha, Waziri wa ardhi alisema, kuanzia mwakani wizara yake itaanza mradi mkubwa wa kupima kila kipande cha ardhi na hati kutolewa kwa mfumo wa kidijitali unaowezesha mwananchi  kumilikishwa hati ya kielektroniki ya kurasa moja.

Akizungumzia suala la urasimishaji makazi katika maeneo mbalimbali nchini,  Waziri Lukuvi aliagiza wananchi wote waliojenga maeneo hatarishi kama vile mabondeni wasirasimishiwe na badala yake maafisa mipango miji waangalie upya ramani zake ili wazirekebishe.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akielekea kuzindua ofisi ya ardhi mkoa wa Geita jana huku akiangalia vifaa vya upimaji wakati wa mfululizo wa uzinduzi wa ofisi za ardhi katika mikoa mbalimbali nchini.

“aliyejenga eneo hatarishi asipewe hati na wapanga miji mrudi kutoa ramani, mvua zimeshusha hadhi yenu na kuonesha mafuriko, futeni katika mpango wenu maeneo yaliyoathirika msiyapange na walio mabondeni wasirasimishiwe” alisema Lukuvi.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Geita Josephat Maganga aliyemwakilisha Mkuu wa mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel alisema kupitia uzinduzi wa ofisi ya ardhi, mkoa huo sasa utafaidi kwa kusogezewa  huduma za sekta ya ardhi karibu ambapo awali zilikuwa zilikuwa zikipatikana ofisi ya kanda uliyokuwemo mkoa wa Mwanza na kutolea mfano upatikanaji hati ulilazimu mwananchi kusafiri hadi Mwanza na kumuingizia gharama.

Mkuu huyo wa wilaya ya Geita alibainisha kuwa, kupatikana kwa huduma zote za sekta ya ardhi katika mkoa wa Geita sasa miji katika mkoa huo itapangika vizuri na maeneo yaliyoiva kimji itapangiliwa vizuri.

Naye Mbunge wa Bukombe ambaye ni Waziri wa Madini Doto Biteko aliishukuru Wizara ya ardhi kwa uamuzi wa kufungua ofisi za ardhi za mikoa pamoja na kutatua migogoro ya ardhi na kubainisha kuwa uzinduzi wa ofisi hiyo ni furaha kwa wana Geita kwa kuwa hatakuwa wakisafiri tena umbali mrefu kufuata huduma ya ardhi Mwanza.

Ad

Unaweza kuangalia pia

MWENDO KASI LEOTakwimu za Sasa za Utekelezaji wa Mradi wa Mwendo Kasi kwa Mwaka 2024

Mradi wa Mwendo Kasi (BRT) nchini Tanzania unaendelea kupiga hatua kubwa katika utekelezaji wake mwaka …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *