WAZIRI DKT. KALEMANI AWACHARUKIA WANAOTOZA BEI KUBWA ZA UMEME

Veronica Simba – Sengerema

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, ametoa onyo kali kwa wazalishaji binafsi wa umeme, wanaowatoza wananchi gharama kubwa tofauti na bei elekezi ya Serikali.

Ad

Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kahunda, wilayani Sengerema, Mkoa wa Mwanza, Julai 7, 2020, Waziri alisisitiza kuwa gharama stahiki ya umeme kwa wananchi wote wenye matumizi ya kawaida ni shilingi 100 tu kwa uniti moja.

Alisema, wananchi wanapaswa kutozwa gharama inayofanana katika maeneo yote nchini kwani wote wana haki sawa.

“Bei hiyo ni kwa maeneo yote nchini vikiwemo visiwa na ni kwa umeme wa aina zote pasipo kujali ni wa TANESCO au kutoka kwa wazalishaji binafsi wanaotumia umeme jua na aina nyinginezo,” alisisitiza Waziri.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (kulia), akieleza dhamira ya ziara yake kwa Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole (kushoto), alipowasili wilayani humo Julai 7, 2020 kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme.

Alitoa agizo kwa viongozi wa Serikali, hususan Wakuu wa Wilaya kote nchini, kuwachukulia hatua wazalishaji binafsi wa umeme, watakaobainika kukiuka mwongozo huo wa Serikali.

Alisema amekuwa akipokea malalamiko kutoka kwa wananchi mbalimbali, hususani wanaoishi visiwani, kwamba wamekuwa wakitozwa gharama kubwa na wawekezaji binafsi wa umeme hali inayosababisha wengi wajisikie kama wakimbizi ndani ya nchi yao.

Waziri alisema kamwe Serikali haitavumilia tabia za aina hiyo zinazooneshwa na baadhi ya wawekezaji binafsi wa umeme kwani imewaamini kutenda haki katika kuwafikishia umeme wananchi hao ambao hawajafikiwa na gridi ya Taifa.

Hata hivyo, alibainisha kuwa Serikali inaendelea na zoezi la kupeleka umeme wa gridi ya Taifa katika visiwa vyote nchini kwa kupitisha nyaya chini ya maji yanayozunguka visiwa hivyo.

Aliwataka wananchi wa visiwani ambao hawajafikiwa na huduma hiyo kuwa watulivu kwani huduma hiyo itawafikia wote awamu kwa awamu.

Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole, akizungumza wakati wa Mkutano wa Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (kushoto) na wananchi wa kijiji cha Kahunda, wilayani Sengerema, Mkoa wa Mwanza (hawapo pichani) Julai 7, 2020. Waziri alikuwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme

Akiwa katika Mkutano huo, Waziri aliagiza kukamatwa na kuhojiwa wawakilishi wa kampuni ya kuzalisha umeme wa jua iitwayo Jumeme, baada ya wananchi wa kisiwa cha Maisome wilayani humo, kuwatuhumu kuwa wamekuwa wakiwauzia umeme kwa gharama ya shilingi 3,500 kwa uniti moja.

Akizungumza katika Mkutano huo wa Waziri, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole, alipongeza hatua za makusudi ambazo Serikali kupitia Wizara ya Nishati, imekuwa ikizichukua katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya umeme.

Aidha, alitoa shukrani na pongezi kwa Serikali, kwa niaba ya wananchi wa Sengerema, kutokana na kutatuliwa kwa changamoto ya kukatika umeme mara kwa mara, iliyokuwa ikiwakosesha amani wananchi hao.

“Umeme sasa haukatiki tena mara kwa mara kama ilivyokuwa awali na hata inapotokea, TANESCO wanatoa taarifa kwa wakati wakieleza sababu za kukata, muda utakaotumika kurejesha huduma hiyo pamoja na maeneo yatakayoathirika,” alisema.

Waziri alikuwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme wilayani humo.

Ad

Unaweza kuangalia pia

RAIS.DKT. SAMIA SULUHU HASSAN AZUNGUMZA NA VYOMBO VYA HABARI KATIKA MJADALA WA KIMATAIFA WA CHAKULA

Katika tukio maalum la Mjadala wa Kimataifa wa Chakula, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *