Tanzania na China zimeahidi kuendeleza ushirikiano wa kidiplomasia ili kuhakikisha kuwa nchi hizo zinakuwa na maendeleo endelevu.
Makubaliano hayo yamefanywa na Balozi wa China nchini, Mhe. Wang Ke, wakati alipokutana kwa mazungumzo na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge leo jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Ibuge amesema kuwa wamejadili masuala mbalimbali ikiwemo suala la namna ya kutekeleza nia ya Viongozi Wakuu wa nchii za China na Tanzania (Rais wa China, Mhe. Xi Jinping pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Joseph Pombe Maufuli) ya kupunguza madhara yatokanayo na ugonjwa wa COVID 19 ikiwemo kufutiwa na kusamehewa madeni.
Naishukuru Serikali ya China kwa uhusiano na ushirikiano ambao imekuwa ikionesha kwa Tanzania. Uhusiano huo umeendelezwa na viongozi wa pande zote mbili ambao umekuwa ukiimarika siku hadi siku na kuahidi kuwa serikali ya Tanzania itaendela kudumisha ushirikiano wake wa kidiplomasia kati yake na China.
Pamoja na mambo mengine, mazungumzo yalijadili masuala ya biashara na uwekezaji, mradi wa nyumba 25 za wataalum wa Afya zilizopo Osterbay jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake Balozi Wang Ke pamoja na mambo mengine, ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa jitihada ilizochukua katika kukukuza uchumi wake hadi kufikia uchumi wa kati, pamoja na mapambano dhidi ya COVID 19.
“Leo nimekutana na Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje, Balozi Brigedia Jenerali Ibuge na kuongea mambo mbalimbali ya ushirikiano na tunaipongeza Serikali ya Tanzania kwa jitihada ilizochukua katika kufanya kazi kwa bidii na kukuza uchumi wake hadi kufikia uchumi wa kati, pamoja na hatua ilizochukua katika kupambana na janga la COVID 19 ambapo tumefurahishwa kuona janga la COVID 19 limeisha,” Amesema Balozi Ke.
Balozi Ke ameongeza kuwa wamekubaliana katika maongezi hayo pia kuendeleza ushirikiano wa kufanya kazi kwa pamoja kwa manufaa ya mataifa mawili (Tanzania na China) ili kuhakikisha uhusiano na ushirikiano unazidi kukua na kuimarika.
Tanzania na China zimekuwa zikishirikiana katika sekta za kilimo, biashara na uwekezaji, miradi ya mikopo nafuu na misaada, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Uchukuzi, Afya, Utalii na utamaduni.
China na Tanzania zilianzisha mahusiano rasmi ya kidiplomasia mwaka 1964.