NEC INATARAJIA KUTANGAZA HIVI KARIBUNI MABADILIKO YA MAJINA KWA BAADHI YA MAJIMBO

Janeth Raphael, Michuzi TV

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), inatarajia kutangaza hivi karibuni mabadiliko ya majina kwa baadhi ya majimbo, huku akisema kuwa inatarajia kutoa ajira kwa watu 390,824 watakaoshiriki usimamizi wake kwenye vituo 75,000.

Ad

Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dkt. Wilson Mahera, aliyasema hayo jana alipohojiwa na Kituo cha Televisheni cha Clouds, akibainisha kuwa katika uchaguzi huo, hakutakuwa na punguzo au nyongeza ya majimbo.Alisema majimbo yatabaki 364. Kati yake, ya Tanzania Bara ni 214 na Zanzibar ni 50 huku kata zikiwa ni 3,956.

“Tume mwaka huu haikuweza kuongeza majimbo, inabaki kuwa na majimbo 214 Bara na 50 Zanzibar na tunaenda kuyatangaza hivi karibuni majina ya majimbo hayo na kata 3,956 kutangazwa, hakuna mabadiliko, mabadiliko yatakayotokea ni majina tu,” alisema.

Kuhusu maandalizi ya uchaguzi huo, Mkurugenzi huyo alisema tume inatarajia kuwa na vituo 75,000 na kila kituo kinakuwa na watu watano.“Hao watu watano ni msimamizi wa kituo cha kupigia kura, anasaidiwa na wasimamizi wawili, karani mwongozaji na mlinzi, hivyo kutakuwa na watumishi 390,824 kwenye vituo hivyo 75,000,” alisema.

Alibainisha kuwa tume inatarajia kutoa tangazo la watu wenye sifa za kusaidia majukumu ya tume kwenye uchaguzi mwishoni mwa mwezi ujao.“Watendaji wote wanaoteuliwa kushiriki masuala ya uchaguzi, tume ina bajeti ya kutoa elimu na kuwajengea uwezo wa kujaza fomu hizo vizuri na tangazo litatangazwa kwenye ngazi ya majimbo, na watakaowafanyia usahili ni ngazi za majimbo,” alisema.

Kuhusu kuchelewa kwa ratiba ya uchaguzi, mkurugenzi huyo alisema tume inafanya majukumu yake kwa mujibu wa sheria na inasubiri tangazo kwenye gazeti la serikali la kuvunja Bunge ndiyo itoe ratiba hiyo.

“Tunasubiria wakati wowote tukishaliona tangazo, ndiyo tume inakuwa na uhuru wa kutoa tarehe ya uchaguzi, na kutangaza ratiba ya uchaguzi na kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi, baada ya kutolewa tangazo la serikali si chini ya siku tano na si zaidi ya siku 25 NEC inabidi itangaze siku ya uteuzi wa wagombea,” alisema na kuwaomba wananchi kuwa na subira hadi tangazo hilo litakapotolewa.

“Haiwezi kufika Desemba na kwa tamaduni za kitanzania, uteuzi umekuwa ukifanyika Agosti na uchaguzi Oktoba, hatujui tunasubiri hiyo siku tukijua tutaita vyombo vya habari kutangaza.

“Hakuna ucheleweshaji wa ratiba maana sheria imetubana, tunasubiri mamlaka ya kuvunja Bunge ionekane kwenye gazeti la serikali na itakapotoka, sheria inakubana kama imetoka tuhesabu siku tano na isizidi siku 25 uwe umefanya uteuzi.”

Ad

Unaweza kuangalia pia

RAIS MHE. SAMIA SULUHU HASSAN AKUTANA NA RAIS WA JAMHURI YA KENYA DKT. WILLIAM SAMOEI RUTO, NAIROBI NCHINI KENYA

Leave a Reply

Your email address will not be published.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.