Kulinda afya kwa kuzingatia mtindo bora wa maisha, ulaji unaofaa, kufanya mazoezi, kuchunguza afya mara kwa mara na kuepukana na mtindo usiofaa wa maisha, ni siri pekee itakayowawezesha Watanzania kufurahia ‘matunda’ Tanzania kuingia nchi zenye Uchumi wa Kati.
Rai hiyo ilitolewa hivi karibuni na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Prof. Mohamed Janabi alipozungumza na waandishi wa habari , katika Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa (SABASABA) na kusisitiza kwamba ni wajibu wa kila mmoja kuendelea kulinda afya yake.
“Nilipoona nchi yetu imeingia Uchumi wa Kati, nilifurahia sana lakini baadae nikakaa na kujiuliza, maana yake ni kwamba wananchi watakuwa na hela nyingi zaidi na wataishi maisha marefu zaidi.
“Inabidi kama nchi tuanze kuwatayarisha sasa hivi kwa kuwaelimisha jinsi ya kuishi maisha bora wakiwa na afya bora, kwa sababu kwa kutokufanya hivyo, tutajikuta wananchi watakuwa na hela nyingi lakini wakazitumia kwa muda mfupi kama hawatachukua tahadhari na kuzingatia kanuni bora za afya ili kuepuka magonjwa,” alisisitiza.
Alisisitiza kwamba yeye pamoja na wataalamu wenzake ambao jumla yao wapo zaidi ya 310 katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete watahakikisha wanaendelea kutoa huduma bora zaidi ya elimu na matibabu dhidi ya magonjwa ya moyo.
“JKCI pamoja na taasisi nyingine za afya ikiwamo MOI, Ocean Road, Hospitali ya Taifa Muhimbili na Hospitali za Kanda, naweza kusema zimechangia kwa kiasi kikubwa nchi kuingia uchumi wa kati.
“Kwa namna gani? Maana yake ni kwamba ukiwa na wananchi wenye afya njema watafanya kazi kwa bidii zaidi, watakuwa na siku chache za kwenda hospitalini, hawataumwa. Ukiwa na wananchi wenye afya njema maana yake umri wa kuishi nao utaongezeka.
“Hii imejihirisha kwa sababu hata umri wa kustaafu nao umeongezwa, kwa wafanyakazi wa kawaida kutoka miaka 55 ya zamani hadi miaka 60 hivi sasa, kwa madaktari bingwa wa binadamu na maprofesa wa vyuo vikuu kutoka miaka 60 hadi miaka 65, ni dhahiri kwamba huduma bora za afya, miundombinu ya afya haiachani na hatua ya nchi kwenda uchumi wa kati na hata kufikia Uchumi wa Juu,” alisisitiza.
Aliongeza “Ikiwa wananchi hawatakuwa na siku za mapumziko (Excuse Duty – ED) kutokana na ugonjwa kila mara, maana yake uchumi utakwenda juu, watazidi kufanya kazi na ndiyo maana sasa kwenye taasisi yetu tuanashauri watu wafanye mazoezi, wazingatie ulaji bora unaofaa, wawe na afya, waweze kufanya kazi kwa bidii ili nchi iweze kuendelea zaidi.