WAKAZI 58,821 KUNUFAIKA NA HUDUMA YA MAJI MKOANI IRINGA

Ukaguzi ukiendelea ujenzi wa tanki la kuifadhia maji

Wakazi 58,821 wa tarafa za Ismani na Kilolo katika Halmashauri za Wilaya za Iringa na Kilolo kwa pamoja wanatarajia kunufaika na huduma ya majisafi na salama pindi Mradi wa Maji Ismani-Kilolo utakapokamilika mwezi Juni, 2021.

Mradi huo unaotekelezwa kwa kutumia wataalam wa ndani kutoka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Iringa (IRUWASA) na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa gharama ya zaidi ya Sh. bilioni 9 unatarajiwa kumaliza changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji kwenye jumla ya vijiji 29 katika tarafa za Ismani (24) na Kilolo (5).

Ad

Akiwa ziarani akikagua Mradi wa Maji wa Ismani-Kilolo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga amewataka wataalam wa IRUWASA na RUWASA kuchukua hatua za dharura kuhakikisha mradi huo unaanza kutoa huduma eneo la Ismani Tarafani ndani ya wiki sita kabla ya mradi mzima kukamilika kwa asilimia 100 ifikapo mwezi Juni, 2021.

“Sikubaliani na mapendekezo yenu kwamba wakazi wa Ismani Tarafani waanze kupata maji hadi ujenzi wa mradi mzima ukamilike wakati hali yao si nzuri, na tuna uwezo wa kuchukua hatua za haraka kuhakikisha wanapata huduma ndani ya muda mfupi,” alisema Mhandisi Sanga.

“Hatua hii ya dharura itagharimu kiasi cha jumla ya Shilingi Milioni 600, ifikapo tarehe 20 Julai mtakuwa tayari mmepokea kiasi cha Shilingi Milioni 200 na utekelezaji uanze mara moja,” alielekeza Mhandisi Sanga.

Mhandisi Sanga alisisitiza maelekezo ya wizara kwa kazi za ujenzi wa miradi yote inayopeleka huduma ya maji kwa wananchi ni lazima ikamilike haraka, kwani Serikali haipo tayari kuona wananchi wakitaabika kwa kukosa huduma ya maji hasa ikizingatiwa kwamba fedha ya utekelezaji wa miradi hiyo ilikwishatengwa.

Aidha, ameridhishwa na maendeleo ya kazi ya upanuzi wa Mradi wa Maji wa Pawaga katika tarafa ya Pawaga, wilayani Iringa na kutoa wiki nne mradi uanze kutoa huduma kwa wananchi kwa sababu kazi iliyobakia ni ndogo.

Ad

Unaweza kuangalia pia

RAIS.DKT. SAMIA SULUHU HASSAN AZUNGUMZA NA VYOMBO VYA HABARI KATIKA MJADALA WA KIMATAIFA WA CHAKULA

Katika tukio maalum la Mjadala wa Kimataifa wa Chakula, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *