Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imetoa sh. bilioni 20 za kulipa madeni ya wakulima, wasafirishaji, wapuliziaji dawa na waendesha maghala ya korosho.
“Rais Magufuli ametoa fedha hizi kwa ajili ya Tandahimba, Masasi, Mtwara na Kibiti kwa ajili ya waliokuwa wamelipwa nusu, waliolipwa kiasi na wasiolipwa kabisa. Fedha hizi zitaanza kulipwa kesho asubuhi,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumapili, Julai 19, 2020) wakati akizungumza na wanachama wa Chama cha Msingi (AMCOS) cha Matogoro na wakazi wa Tandahimba mkoani Mtwara alikoenda kuhamasisha maandalizi ya msimu wa ununuzi wa korosho.
Amesema uhakiki uliofanywa kwa wakulima wa Kibiti, Rufiji, Mkuranga, Ruangwa, Liwale, Lindi, Tunduru na wilaya zote za mkoa wa Mtwara ulibaini kuwa wakulima na watoa huduma wote walikuwa wakidai zaidi ya sh. bilioni 23.
“Katika hao, Tandahimba wanadai zaidi ya sh. bilioni 9, Masasi wanadai sh. bilioni 2.3 na Mtwara Vijijini wanadai sh. milioni 884. Nyingine ni za Pwani na Lindi,” amefafanua.
Waziri Mkuu amesema fedha hizo zimetokana na mfumo uliotengenezwa na wanunuzi ili kumnyonya mkulima katika msimu wa 2018/2019 kwa kununua kilo ya korosho kwa sh. 1,500 badala ya sh. 3,000 hali iliyolazimu Serikali kuingilia kati na kuamua kuzinunua korosho zote.
Waziri Mkuu alishuhudia Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Kilimo (TABD), Bw. Japhet Justine akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Bw. Gelasius Byakanwa hundi ya sh. 9,050, 846,030 ambaye pia aliikabidhi kwa viongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Tandahimba na Newala (TANECU) na AMCOS ya Matogoro.
Awali, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mtwara, Bw. Yusuph Nanila alimuomba Waziri Mkuu atoe majibu ya lini wakulima wa Tandahimba watalipwa fedha zao, ambazo zimefikia zaidi ya sh. bilioni 9.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amevitaka Vyama Vikuu vya Ushirika na AMCOS waweke kipaumbele cha kununua mashine ndogo ndogo za kubangulia korosho ili waache mtindo wa kuuza korosho ghafi.
“Ukibangua kilo tatu za korosho yenye maganda, unapata kilo moja ya korosho zilizobanguliwa. Kilo moja ya korosho yenye maganda inauzwa sh. 2,400 kwa hiyo kilo tatu ni sh.7,200, lakini ukizibangua, kilo moja inauzwa sh.25,000. Ninawasihi tuanzishe viwanda vidogo vya kubangua korosho ili tupate fedha zaidi kwenye vyama vya msingi.”
“Matogoro mnaweza kununua hata mashine 100 kutoka SIDO ili mzibangue hapahapa na kuongeza pato la wakulima wenu. Tena mashine za viwanda vidogovidogo zinatoa korosho nzuri zenye ubora sawa na zilizotoka kwenye mashine kubwa,” aliongeza.
Kuhusu msimu wa ununuzi wa korosho, Waziri Mkuu alisema msimu mpya unaanza Septemba hadi Desemba na akawataka viongozi wa ushirika wasimamie ununuzi wa korosho mapema.
Aliwataka wakulima wa korosho wa wilaya hiyo wabadili mfumo wa kilimo cha zao hilo kwa kuanza kupanda miche mipya ambayo inazaa kwa wingi na inachukua muda mfupi kukomaa. “Pandeni miche mipya kwa sababu inazaa ndani ya mwaka mmoja na nusu, ondoeni mikorosho iliyozeeka.”
Pia aliwataka wanachama hao walime mazao mbadala kama chikichi na alizeti ambayo yanakubali kwenye ardhi yao ili waongeze wigo wa sgughuli za kiuchumi kwenye wilaya hiyo. “Michikichi inakubali sana kwenye ukanda wa pwani, kwa hiyo jaribuni muone ukuaji wake.”
Kuhusu malipo ya wasafirishaji, Waziri Mkuu alisema kati ya fedha zilizolipwa, wasafirishaji wametengewa sh. bilioni 3.3. Alikuwa akijibu swali la Mwenyekiti wa Chama cha Wasafirishaji wilayani Tandahimba, Bw. Maulid Mussa ambaye alisema walisafirisha korosho kutoka kwa wakulima hadi kwenye maghala na madai yao yaliyofikia sh. milioni 600 yamekuwa yakiwanyima usingizi kwa muda mrefu.
Kuhusu bei dira ya korosho, Waziri Mkuu amewaelekeza viongozi wa vyama vya msingi na vyama vikuu nchini kote wakae na kuandaa gharama ambazo mkulima anakuwa amezitumia na gharama zitakazokubaliwa ndiyo iwe msingi wa bei dira.
“Vyama vikuu vifanye hiyo kazi kabla msimu haujaanza Septemba 2020. Mniletee ofisni kwa maandishi ili tumshirikishe Waziri wa Kilimo na kisha tutangaze kitaifa bei dira ni ipi,” amesema.