Tanzania katika kuhakikisha inatimiza azma ya kuwa nchi ya viwanda na kujitosheleza kwa bidhaa ndani ya nchi imedhamiria kuwekeza kwenye uzalishaji wa ndani.
Akizungumzia sekta ya afya, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Bw. Adam Fimbo amebainisha kuwa katika miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Magufuli nchi imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuanzisha viwanda vya dawa, vifaa tiba na vitendanishi.
Katika maelezo yake wakati akifunga mkutano wa wahariri wa vyombo vya habari uliofanyika leo mjini Morogoro, Fimbo alisema muda mfupi Tanzania itakuwa na viwanda visivyopungua 30 baada ya wawekezaji kujitokeza kwa wingi kuanzisha viwanda vya dawa na vifaa tiba.
“Takwimu za nyuma zinaonyesha Tanzania inaingiza zaidi dawa na vifaa tiba kuliko zile zinazozalishwa nchini, inaonekana asilimia 10 tu ya dawa na vifaa tiba ndiyo inazalishwa nchini asilimia 90 tunaagiza. Lakini hii ni kwa mujibu wa utafiti uliofanyika mwaka 2016.
“Miaka imesogea na uwekezaji katika sekta ya afya umekua. Naamini utafiti ukifanyika sasa hali itakuwa tofauti na hivyo. Hadi sasa tuna viwanda 14 na viwanda 16 vipo katika hatua za mwisho kukamilika ujenzi ili kuanza uzalishaji. Utaona hii asilimia ya uagizaji itashuka,” alisema Fimbo.
Awali akiwasilisha mada ya mchango wa TFDA katika kutekeleza sera ya viwanda,Kaimu Mkurugenzi wa Dawa na Vifaa tiba Bwa.Akida Khea alisema wawekezaji wa ndani wamepata mwamko mkubwa katika kuziba ombwe la uagizaji dawa.
“Kati ya wawekezaji 16 waliokuja kuomba kujenga viwanda vya dawa na vifaa tiba, ambaye si Mtanzania ni mmoja tu. Maana yake wawekezaji 15 ni Watanzania. Hii itatusaidia kukuza kipato cha nchi na kuongeza ajira,” alisema Khea na kuongeza:
“Tumehakikisha wanafuata taratibu zote za uanzishaji viwanda vya namna hii. Tumekuwa tukiwatembelea mara kwa mara ili kuhakikisha hawakiuki sheria kwa kuwa haya ni maisha ya watu tutambue dawa ni sumu ukiitumia vibaya inakudhuru.”
Aidha, katika semina hiyo ya siku moja iliyokuwa na malengo ya kuongeza uelewa wa wanahabari kwenye masuala ya kanuni na taratibu zinazowaongoza TFDA kuhakikisha wananchi wanakuwa salama, maazimio yaliyowekwa ni kuongeza ushirikiano kati ya wanahabari na taasisi hiyo lakini pia kuongeza ukali kwa watu wanaotoa matangazo yanayopotosha umma juu ya dawa zisizofaa. Michuzi Blog