BALOZI WRIGHT – MAREKANI INAIONA TANZANIA NI NCHI IMARA, TULIVU NA YENYE DEMOKRASIA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 02 Agosti, 2020 amepokea Hati za Utambulisho za Mabalozi 2 walioteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa Tanzania.

Balozi wa Marekani hapa nchini Donald John Wright akiwa amesimama wakati nyimbo za Mataifa mawili ya Tanzania na Marekani zilipokuwa zikipigwa na Brass Band ya Polisi katika mapokezi yake Ikulu jijini Dar es Salaam.

Waliowasilisha hati hizo Ikulu Jijini Dar es Salaam ni Mhe. Dkt. Donald John Wright aliyeteuliwa kuwa Balozi wa Marekani hapa nchini na Mhe. Nguyen Nam Tien, aliyeteuliwa kuwa Balozi wa Vietnam hapa nchini.

Ad

Katika mazungumzo baada ya kupokea hati hizo, Rais Magufuli amewakaribisha Mabalozi hao hapa nchini na ameeleza kuwa Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano mzuri na wa kihistoria uliopo kati yake na nchi hizo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi katika picha ya pamoja na Balozi wa Marekani hapa nchini Donald John Wright Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais Magufuli amewaomba Mabalozi hao kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchini mwao kuja kuwekeza hapa nchini na kwamba Serikali itakuwa tayari wakati wowote kutoa ushirikiano kwao.

Akizungumza baada ya kuwasilisha hati zake za utambulisho, Balozi Wright ameeleza kufurahishwa kwake na kurejea Tanzania baada ya miaka 33 tangu alipokuja kwa mara ya kwanza kufanya kazi za kutoa matibabu, na kwamba tangu wakati huo anawaheshimu na kuwapenda Watanzania kutokana na ukarimu wao, upendo wao na jinsi wanavyoishi na wageni kama wanafamilia wao.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Marekani hapa nchini Donald John Wright mara baada ya kuwasilisha Hati za Utambulisho kwake katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Balozi Wright amesema Marekani inaiona Tanzania ni nchi imara, tulivu na yenye demokrasia, na kwamba uhusiano wake mzuri na Marekani umeiwezesha kufanya kazi pamoja na anatarajia kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano zaidi na Serikali ya Tanzania.

Pia, Mhe. Balozi Wright amewasilisha salamu za rambirambi kwa Mhe. Rais Magufuli kutoka kwa Rais wa Marekani Mhe. Donald Trump na Serikali ya Marekani kufuatia kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Hayati Benjamin William Mkapa na kueleza kuwa Marekani inatambua mchango mkubwa wa Hayati Mkapa kwa Tanzania na Kimataifa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi katika picha ya pamoja na Balozi wa Viet Nam hapa nchini Nguyen Nam Tien mara baada ya kuwasilisha Hati za Utambulisho kwake katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Nae Mhe. Nguyen Nam Tien amesema Tanzania ni nchi nzuri, Rais wake anafanya kazi nzuri na kwamba anatazamia kuendelea kufanya kazi kwa ukaribu zaidi ili kukuza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano uliopo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi ameelezea uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Marekani na kwamba Marekani imekuwa ikifadhili miradi mingi akiwemo afya  ambapo imetoa Shilingi Trilioni 1.56 mwaka 2018, miradi 3,179 ya uwekezaji kutoka Marekani ambayo imezalisha ajira 550,000 kwa Watanzania, na pia mauzo ya bidhaa za Tanzania nchini Marekani yamekuwa yakiongezeka ambapo mwaka 2019 bidhaa zenye thamani ya shilingi Bilioni 119 ziliuzwa nchini Marekani.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akimsikiliza Balozi wa Viet Nam hapa nchini Nguyen Nam Tien mara baada ya kuwasilisha Hati za Utambulisho kwake katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

“Kwa hiyo uhusiano wa Tanzania na Marekani ni mzuri na unazidi kuimarika na tunaamini kuwa kuja kwa Mhe. Balozi Donald John Wright kutaimarisha zaidi uhusiano huo” amesema Prof. Kabudi.

Kwa upande wa Vietnam, Mhe. Prof, Kabudi amesema Tanzania imekuwa na uhusiano wa kidugu na kihistoria na nchi hiyo ambapo inashirikiana nayo katika mambo mengi ikiwemo uwekezaji wa kampuni ya simu za mkononi ya Halotel.

Ad

Unaweza kuangalia pia

Je! Wajua Mchango wa Madini ya Tanzanite katika Pato la Taifa?

Madini ya Tanzanite, yanayopatikana pekee katika eneo dogo la Mererani, Tanzania, ni miongoni mwa rasilimali …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *