Serikali imekabidhiwa jiwe lingine la tanzanite lenye uzito wa kilo 6.3317 lililopatikana katika mgodi wake wa mfanyabiashara Saniniu Laizer uliopo katika kitalu D ndani ya ukuta unaozunguka machimbo hayo ya madini adhimu duniani.
Jiwe hili ni la tatu kupatikana na kuuzwa Serikalini baada ya mawe mengine mawili kununuliwa na serikali katika hafla iliyofanyika tarehe 24 Juni, 2020 mara baada ya mchimbaji huyo kuiarifu Serikali juu ya uwepo wa mawe mawili yenye uzito mkubwa yaliyochimbwa mgodini kwake mnamo tarehe 17 Juni, 2020 yaliyokuwa na thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 7.
Imeelezwa kwamba ndani ya muda mfupi baada ya Serikali kununua madini hayo kutoka kwa mchimbaji huyo mdogo, mchimbaji huyo alitoa tarifa ya kupatikana kwa jiwe lingine ambapo Serikali imeridhia kununua jiwe hilo na kuifanya Serikali kuwa na mawe matatu ya tanzanite yenye uzito mkubwa kwa uzito wa kufuatana ambapo zito zaidi lina kilo 9.27, kilo 6.33 na kilo 5.103.
Akizungumza wakati wa hafla iliyofanyika tarehe 03 Agosti, 2020, Waziri wa Madini, Doto Biteko aliwataka wachimbaji wadogo wa madini kuacha tabia ya kutorosha madini na kueleza kuwa tabia hiyo haina faida yeyote kwao na zaidi itawasababishia hasara kubwa na kuwapelekea kukamatwa na kushughulikiwa na vyombo vya dola.