NAIBU WAZIRI SIMA ASISITIZA ULINZI KATIKA VYANZO VYA MAJI

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima akitoa maelekezo akiwa katika banio la banio la mfereji wa Mnazi katika Kijiji cha Warumba, Kata ya Imalilo Wilayani Mbarali baada ya kukagua changamoto za matumizi ya maji katika eneo hilo. Kutoka kulia ni Prof Esnat Chaggu Mwenyekiti wa Bodi – Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC, Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Reuben Mfune, Izumbe Msindai Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa uhifadhi – Hifadhi ya Taifa Ruaha na Dkt. Samuel Gwamaka Mkurugenzi Mkuu -NEMC

Na Lulu Mussa, Mbarali

Serikali imesema itahakikisha kuwa vyanzo vya maji vinavyopeleka maji Mto Rufiji havivamiwi kwa shughuli za kibinadamu ili Mradi Mkubwa wa kufua umeme katika bonde la Mto Rufiji uweze kutekelezeka.

Ad

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mussa Sima mara baada ya kukagua maeneo yenye changamoto za kimazingira pamoja na kutafuta ufumbuzi kwenye ikolojia ya vyanzo vya maji vinavyo changia maji katika bonde la Rufiji.

Akiwa Wilayani Mbarali Mkoani Mbeya Naibu Waziri Sima ametembelea banio la mfereji wa Mnazi katika Kijiji cha Warumba, Kata ya Imalilo ambalo linachangia upotevu wa maji kwakuwa liko katika kona ya mto ambapo maji mengi huacha mto na kuelekea katika mfereji na kuathiri ikolojia ya mto.

Naibu Waziri Sima ametoa wito kwa wananchi kutoharibu vyanzo ili kuwa na maji ya kutosha kutekeleza mradi huo mkubwa wa uzalishaji wa umeme katika Bonde la mto Rufiji. “Mito hii ya Ruaha Mkuu, Kilombero na Luegu inapoungana ndio inatengeneza Mto Rufiji ambako ndiko kuna maporomoko ya “Stiglers Gorge” hivyo ni vema wananchi wakapewa elimu ya kutosha ya kufanya kilimo endelevu na kuwa na matumizi mazuri ya maji ili mradi mkubwa wa ufuaji umeme ufanikiwe na kilimo kiendelee” Sima alisisitiza.

Katika ziara yake Naibu Waziri Sima ameweza kutoa miongozo muhimu yenye kukuza, kulinda na kusimamia mazingira kwa namna endelevu husunan Ikolojia ya Vyanzo vya maji katika Mikoa aliyopita. “Tuendelea kuelimisha wananchi juu ya upandaji miti rafiki wa mazingira na kuepuka kilimo kandokando ya mito ili kulinda mazingira yetu. Wananchi ndio walinzi na wahifadhi wa kwanza katika kutunza Mazingira” Sima alibainisha.

Naibu Waziri Sima amesema Sheria ya Mazingira, 2004 kifungu cha 6 kimetamka wajibu wa kila mwananchi kutunza Mazingira hivyo mtu yeyote anayeishi Tanzania ni  mdau na atawajibika kutunza na kuendeleza Mazingira na kutoa taarifa kwa mamlaka husika kuhusu shughuli au jambo lolote ambalo kwa kiasi kikubwa linaweza kuathiri mazingira. Hivyo kupitia sheria hii si jukumu la Serikali pekee kusimamia uhifadhi wa Mazingira, wananchi nao wana wajibu wa moja kwa moja wa  kutunza Mazingira.

Kwa upande mwingine Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Nchini Dkt. Samuel Gwamaka alieambatana na Naibu Waziri Sima katika ziara hiyo amesema kuwa Baraza litashirikiana  na uongozi wa Wilaya ya Mbarali kuhakikisha kuwa matumizi ya rasilimali ya maji yakuwa endelevu.

Ad

Unaweza kuangalia pia

Mradi wa Magari ya Mwendo Kasi, Kuboresha Usafiri, Uchumi, na Mazingira Tanzania

Mradi wa magari ya mwendo kasi nchini Tanzania umekuwa na faida nyingi za kijamii, kiuchumi, …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *