DCIM100MEDIADJI_0022.JPG

RAIS MAGUFULI ABADILISHA AHADI KUWA VITENDO NDANI YA MIAKA MITANO YA UONGOZI WAKE

Na,ZYNABU ABDULMASOUDI, DODOMA.

Kuna usemi wa Kiswahili unaosema ahadi ni deni,ukimaanisha kuwa unapoweka ahadi huna budi kuitimiza.

Ad

Ahadi iliyowekwa na Rais Dk.John Magufuli wakati wa kampeni zake za kugombea Urais miaka mitano iliyopita ikiwemo ya kutoa elimu bila ya malipo kwa wanafunzi wa darasa la kwanza hadi kidato cha nne imetimizwa na manufaa yake yameonekana.

“Natambua watanzania pamoja na kutaka afya bora, mnatamani mpate elimu nzuri ,hakuna mtanzania ambaye ana mtoto wake amemuhangaikia amemtunza lakini anapoenda shuleni anafukuzwa kwa sabau ya karo au anapoenda shule hana kiti cha kukalia,mwanafunzi wa chuo kikuu anapoenda hapati mkopo na swala lenyewe ni mkopo, nataka haya niyamalize mimi,

Anaongeza kusema kuwa, “Na watu wanasema msema kweli ni mpenzi wa Mungu,mimi siwezi kusimama hapa nikasema uwongo,ninachosema nina uhakika nacho na uwezo wa kukitenda ninao,hiyo ndio Tanzania ninayotaka kuijenga,hiyo ndio Tanzania ninayotaka kuiletea mabadiliko,”anasisitiza Dk Magufuli.

Utekelezaji wa ahadi ya Rais Magufuli katika sekta ya elimu sio tu umepelekea uwepo wa mwamko wa wazazi kuwapeleka watoto wao shule bali umeleta ongezeko kubwa la wanafunzi wanaoandikishwa darasa la kwanza na wale wanaoendelea na kidato cha nne.

Akizungumza na makala hii,Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Selemani Jafo anasema katika kipindi cha kuanzia mwezi Desemba, 2015 hadi Juni, 2020, Serikali imetumia jumla ya Shilingi Trilioni 1.09 kugharamia Mpango wa Elimumsingi Bila Malipo.

Anasema kati ya fedha hizo kiasi cha Shilingi Bilioni 502.2 kimetumika kwa Shule za Msingi na Shilingi Bilioni 593.9 kwa shule za Sekondari kwa ajili ya chakula kwa wanafunzi wa bweni, chakula kwa wanafunzi wa kutwa kwa shule zenye wanafunzi wenye mahitaji maalum, ruzuku ya uendeshaji ,fidia ya ada kwa wanafunzi na posho ya Madaraka kwa Maafisa Elimu Kata na Wakuu wa Shule za Msingi na Sekondari.

Anataja mafaniko yaliyopatikana katika utoaji wa elimu msingi bila ya malipo kuwa ni kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi walioandikishwa kutoka Mil 10,201,972 mwaka 2015 hadi milioni 12,034,599 mwaka 2020.

Aidha upande wa shule ya sekondari anasema idadi ya wanafunzi imeongezeka kutoka 1,806,955 mwaka 2016 hadi 2,023,457 mwaka 2020.

Pia wanafunzi wanaochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wameongezeka kutoka asilimia 60 mwaka 2015 hadi asilimia 100 mwaka 2020,ambapo wanafunzi wote 759,737 waliofaulu mtihani wa kumaliza elimu ya msingi wakiwemo wanafunzi 1,342 wenye mahitaji maalum walichaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza.

 “Haya ndio matokeo chanya aliyoyakusudia Rais wetu Dk Magufuli wakati anaomba kura,na katika hili tunamshukuru sana kwa kuwa mpango huu umewawezesha wanafunzi wengi zaidi hasa wanaotoka katika familia duni kupata fursa ya kwenda shule,”anasema waziri Jafo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu TAMISEMI,mhandisi Joseph Nyamhanga anasema utoaji wa Elimumsingi bila Malipo unazingatia Ibara ya 3.1.5 ya Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 na Ibara ya 52(a) ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015.

Anasema dhana ya Elimumsingi bila Malipo inazingatia uendeshaji wa shule bila ada wala michango ya aina yoyote ya lazima kutoka kwa wazazi au walezi wa wanafunzi.

Mhandisi Nyamhanga anasema mpango huo ni moja ya mikakati waliyoiweka katika kufikia malengo hayo kwa kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa wanafunzi ili kufanya uwe fanisi zaidi na wenye kuzingatia mahitaji ya kila mwanafunzi.

Anataja mikakati mingine kuwa ni  kujenga, kukamilisha na kukarabati miundombinu ya shule,kuendelea kutoa ajira kwa walimu,kutoa mafunzo kazini kwa walimu na viongozi wa elimu.

Nae,Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI anayeshughulikia Elimu Gerald Mweli anasema katika kipindi cha kuanzia Desemba, 2015 hadi Juni, 2020 jumla ya Shilingi Bil 501.78 zimetumika kujenga, kukamilisha na kukarabati miundombinu ya elimu katika shule za Msingi na Sekondari.

Anataja miundombinu iliyojengwa kuwa ni pamoja na vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, mabwalo ya chakula,matundu ya vyoo, maabara, maktaba, mabweni na majengo ya utawala.

“Ujenzi wa miundombinu hii umetokana na utekelezaji wa Programu mbalimbali zikiwemo EP4R, LANES, EQUIP-T na Programu Endelevu ya usambazaji wa Maji Vijijini na Usafi wa Mazingira (SRWSS),”anasema Mweri.

Anasema hadi kufikia mwezi Juni 2020 ujenzi wa shule mpya za Msingi 905 ulikuwa umekamilika hivyo kuongeza idadi ya shule za Msingi kutoka 16,899 mwaka 2015 hadi 17,804 mwaka 2020.

Pia vyumba vya madarasa 17,215 vimejengwa na kuongezeka kutoka vyumba 108,504 mwaka 2016 hadi 125,719 mwaka 2020, sawa na ongezeko la asilimia 13.7 ambapo ujenzi wa vyumba 3,049 unaendelea na ukikamilika idadi ya vyumba vya madarasa kwa shule za Msingi itafikia 128,768.

Upande wa madawati anasema serikali imepunguza kwa kiasi kikubwa uhaba wa madawati na kuwa na jumla ya madawati 5,070,896 na hivyo kuongeza idadi ya madawati kutoka madawati 3,024,311 mwaka 2015 hadi kufikia 8,095,207 sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 200.

Upande wa shule za sekondari anasema serikali imejenga shule mpya za Sekondari 228 na hivyo kuongezeka kutoka shule 4,708 mwaka 2016 hadi 5,330 mwaka 2020.

Anasema vyumba 227 vya maabara za masomo ya Sayansi vimekamilishwa kwa gharama ya Sh. Bilioni 2.63,ujenzi ambao umeongeza idadi ya vyumba vya maabara kutoka 4,237 mwaka 2015 hadi 4,464 mwaka 2020.

Mweli anasema uwekezaji na maboresho yaliyofanyika katika sekta ya elimu kwa shule za msingi na sekondari umesaidia kuongeza kiwango cha ufaulu katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kutoka asilimia 67.84 mwaka 2015 hadi asilimia 81.50 mwaka 2019.

Upande wa elimu ya sekondari anasema katika mtihani wa Taifa wa kidato cha nne, ufaulu umeongezeka kutoka asilimia 67.9 mwaka 2015 hadi asilimia 80.65 mwaka 2019.

“Matokeo ya mtihani wa Taifa wa kidato cha Sita mwaka 2019 yameonesha kuwa katika shule 100 zilizofanya vizuri zaidi Kitaifa, jumla ya shule 64 sawa na asilimia 64 ni za Serikali na Shule 36 sawa na asilimia 36ni shule zinazomilikiwa na taasisi Binafsi.

WANANCHI WANENA.

Mkazi wa Mpwapwa Maria Chiduyu anamtaja Rais Magufuli kama shujaa wake aliyerudisha ndoto alizokuwa nazo kijana wake katika elimu.

“Niliolewa miaka 34 iliyopita,nimeishi na mume wangu akiwa ndio mtafutaji katika familia yetu,lakini alituacha miaka 10 iliyopita na mtoto wetu kulazimika kukaa nyumbani pasipo kwenda shule,lakini shujaa wangu Magufuli akarudisha matumaini yetu,kwa kweli tunamshukuru sana,”anasema mwananchi huyo.

Ad

Unaweza kuangalia pia

RAIS.DKT. SAMIA SULUHU HASSAN AZUNGUMZA NA VYOMBO VYA HABARI KATIKA MJADALA WA KIMATAIFA WA CHAKULA

Katika tukio maalum la Mjadala wa Kimataifa wa Chakula, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *