Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Abdul-Razaq Badru amewataka watumishi wa Ofisi hiyo kufanya kazi kwa bidi, maarifa na nidhamu kwa wateja wake ili kukidhi matarajio ya utoaji huduma bora kwa wanafunzi waombaji na warejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu nchini.
Akizingumza jana Jumanne (Agosti 18, 2020) Jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa mafunzo elekezi kwa watumishi wapya waliohamia HESLB katika kipindi cha miezi sita iliyopita, Badru alisema kila mtumishi ndani ya HESLB anapaswa kutoa huduma bora kwa wateja kwani ndiyo wajibu wa msingi wa mtumishi wa umma.
Badru alisema wateja ndio msingi mkuu wa uwepo wa taasisi yoyote ya umma, hivyo ni wajibu wa watumishi wa HESLB kuhakikisha inawadumia vyema wateja wote wanaofika katika ofisini hapo, ambapo sehemu kubwa ni pamoja na wanafunzi waombaji mikopo na waliokuwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu.
‘Wateja wetu ndio watu wanaotuweka mjini, hawa ndio msingi wa uwepo wetu, tunapaswa kuwahudumia vyema, tusiwe kikwazo kwa wateja kupata huduma, tufanye kazi kwa nidhamu katika kutekeleza majukumu katika maeneo yetu ya kazi’’ alisema Badru.
Akifafanua Zaidi, Badru alisema ni wajibu wa watumishi hao wapya kujituma katika maeneo yao ya kazi na kuwapongeza kuhamia HESLB kwa kuwa taasisi hiyo inatumia mifumo mbalimbali ya kupima walionao katika kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa utaratibu ikiwemo kutumia Mfumo wa Wazi wa Mapitio na Tathmini ya Utendaji Kazi (OPRAS).
Aidha Badru aliwaka watumishi wa Ofisi hiyo kutunza rasilimali za umma ikiwemo vifaa na vitendea kazi vinavyotolewa na Serikali kwa ajili ya matumizi ya ofisi hiyo na kuongeza kuwa watumishi wote kuendelea kushirikiana katika usimamizi wa rasilimali hizo ili ziwe na matumizi endelevu kwa manufaa ya taasisi hiyo.
Kwa upande wake Mkufunzi wa Mafunzo hayo kutoka, Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Mariam Muhenga alisema utoaji wa huduma bora kwa wateja ni moja ya misingi ya kanuni za maadili ya utumishi wa umma, hivyo ni wajibu wa mtumishi wa HESLB kuhakikisha kuwa anasimamia kanuni hizo ili kuleta tija katika maeneo ya kazi.
Aliongeza kuwa mtumishi wa umma ni kioo katika jamii, hivyo anapaswa kuzingatia kuwa mfano wa kutazamwa katika taswira chanya wakati wote anapokuwa anatekeleza wajibu wake katika kutoa huduma kwa wateja.